Mchungaji Mono amrithi Sendoro Dayosisi ya Mwanga

Mwanga. Msaidizi wa askofu wa Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria (DKMZV), Mchungaji Daniel Mono amechaguliwa kuwa mkuu mteule wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Dk Mono amechaguliwa leo Machi 10, 2025 katika mkutano mkuu maalumu uliofanyika katika Kanisa Kuu la Dayosisi ya Mwanga, bila mwenyewe kuwepo.

Katika uchaguzi huo, ambao umesimamiwa na Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dk Alex Malasusa, Dk Mono alikuwa mgombea pekee na wajumbe ama walipiga kura ya Ndiyo au ya Hapana.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Dk Malasusa amesema Dk Mono amepata kura 127 za Ndiyo sawa na asilimia 96.2, kati ya kura 132 zilizopigwa, huku kura za Hapana zikiwa tano.

Dayosisi ya Mwanga imefanya uchaguzi wa askofu ikiwa imepita miezi sita tangu Askofu Dk Chediel Sendoro afariki dunia kwa ajali na hivyo nafasi hiyo kubaki wazi.

Mkuu wa KKKT Dk Alex Malasusa akizungumza katika mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi wa Askofu Dayosisi ya Mwanga

Askofu Sendoro ambaye alihudumu kama Askofu wa Mwanga kwa miaka minane, alifariki dunia Septemba 9, 2024 katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.

Askofu Sendoro alikuwa askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga aliyeingizwa kazini Novemba 6, 2016 baada ya kuzaliwa kwa dayosisi hiyo, iliyotokana na kugawanywa kwa Dayosisi ya Pare iliyokuwa na mgogoro wa muda mrefu.

Viongozi waliohudhuria katika mkutano wa uchaguzi huo ni Waziri mkuu mstaafu Cleopa Msuya, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mwanahamis Munkunda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga, Zahara Msangi na Mbunge wa Mwanga, Joseph Thadayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *