
Kibaha. Imeelezwa kuwa uwepo wa vijana waliokosa maadili mema ndani ya jamii kunasababishwa na wazazi wao kushindwa kusimamia malezi na makuzi bora kwa watoto.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Aprili 21, 2025 na mchungaji kutoka Kanisa la Anglikana Mtakatifu Gabriel Kibaha Pwani, Reymond Mwegoha kabla ya kutoa huduma ya ubatizo kwa watoto wakati wa ibada ya Jumatatu ya Pasaka.
“Watoto hawawezi kufanya dhambi bila kuwaona wazazi wanafanya dhambi kwa kuwa wanajifunza kwa wazazi wao, hivyo ili kuepusha hayo yasitokee wazazi na walezi mnapaswa kuishi maisha yenye maadili mema,” amesema.
Mwegoha ambaye ni mchungaji mstaafu ndani ya Kanisa Anglikana amesema kuwa katika utumishi wake wa kipindi kirefu ndani ya kanisa ameshuhudia mambo mengi ikiwamo baadhi ya vijana kuishi maisha yasiyostahili hasa kujihusisha na vitendo viovu.
“Hivi niwaulize wazazi ikiwa mtoto atashuhudia vitendo vizuri kutoka kwenu tangu utoto wake hadi kuwa mtu mzima ataamzia wapi kujihusisha na ulevi, wizi au hata uasherati,” amehoji Mwegoha.
“Kinachowayumbisha watoto na kujikuta wanatumbukia kwenye mambo ya hovyo ni baadhi ya wazazi wao kutosimama kimaadili.”
Amewataka wazazi waliojitokeza kuwadhamini watoto kuingia daraja la ubatizo kuwa mfano bora na kielelezo kizuri ili kuigwa na kundi hilo changa linalotegemewa na jamii kuanzia ngazi ya familia na Taifa kwa miaka ijayo.
Stella Jonas, mmoja wa waumini wa kanisa hilo amesema jamii inajengwa na wazazi hasa wakishikamana kulea watoto wao kwa ukamilifu.
“Wazazi wanapaswa kuwa wamoja katika malezi na matunzo, lakini asilimia kubwa jamii hivi sasa imejikita katika matunzo pekee na kusahau malezi ambayo ni muhimu kwa watoto,” amesema.
Muumini mwingine, Joyce Ulembo yeye amesema ni vyema jamii ikazingatia wajibu wa kulea na kutunza watoto ili kukuza kizazi chenye faida kwa familia na Taifa kwa jumla.
“Sasa kama baba akiwa ananunua chakula na mahitaji mengine kwa familia yake lakini hazingatii malezi bora, huyo hana tofauti na mfugaji wa mbuzi ambaye anaangalia wamekula na wamelala tu. Kufanya hivyo matokeo yake ni mabaya kwa kuwa anakuza kizazi kisicho na maadili mema,” amesema.