
Singida. Mahakama ya Rufani imemuachia huru mchunga mifugo, Jumanne Yohana aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumlawiti mtoto wa kiume wa waajiri wake aliyekuwa na umri wa miaka mitatu.
Awali mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, ilielezwa tukio hilo lilitokea Juni 20, 2017 ,eneo la Ruvu darajani ambapo mrufani huyo alidaiwa kukutwa na mwajiri wake akimlawiti mtoto huyo.
Hii ni rufaa yake ya pili ambapo jopo la majaji watatu ambao ni Zepharine Galeba, Patricia Fikirini na Mustafa Ismail, walioketi Dar es Salaam walitoa hukumu hiyo iliyomuachia huru Aprili 28,2025.
Kupitia nakala ya hukumu hiyo iliyowekwa kwenye mtandao wa Mahakama, Majaji hao baada ya kupitia mwenendo, kumbukumbu za rufaa na sababu za rufaa hiyo, wamebaini mapungufu katika ushahidi wa mashahidi wanne wa mashitaka waliotoa ushahidi katika kesi ya msingi.
Jaji amesema baada ya kupitia kumbukumbu hizo, wanaunga mkono hoja ya saba ya rufaa kwamba kesi hiyo haikuthibitishwa bila shaka yoyote, hivyo kufuta hukumu dhidi ya mrufani huyo na kuweka kando adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na kuamuru aachiwe huru.
Ilivyokuwa
Wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi, mama wa mtoto huyo ambaye alikuwa shahidi wa kwanza, aliieleza Mahakama kuwa alimkuta Jumanne akimlawiti mtoto wake.
Katika kesi hiyo ya jinai ya mwaka 2017, Jumanne alisomewa kosa la ulawiti kinyume na kifungu cha 154 (1) (a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu ambapo baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili ilimkuta na hatia na kumuhukumu adhabu hiyo.
Baada ya kutoridhishwa na hukumu hiyo, Jumanne alikata rufaa Mahakama Kuu ambapo rufaa hiyo ilisikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, baada ya Hakimu kuongezewa mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.
Ilivyokuwa
Shahidi wa kwanza alidai kumkuta Jumanne akimlawiti mtoto wake jambo lililomlazimu kumpigia simu mumewe (shahidi wa tatu), ambaye alidai kuwa mrufani alikiri kutenda kosa hilo.
Shahidi wa tatu, alieleza kuwa alitumia tochi kummulika mtoto kwenye sehemu ya haja kubwa ambapo aliona manii, ambaye aliongeza kuwa yeye na majirani waliompeleka mwathiriwa hospitalini kwa uchunguzi wa kiafya, baada ya kupata PF3 kutoka kwa polisi.
Shahidi wa nne, Dk Gilbert Daudi aliyemfanyia uchunguzi wa kimatibabu mtoto huyo alieleza kuwa alimkuta na mbegu za kiume kwenye nguo zake pamoja na michubuko kwenye sehemu yake ya haja kubwa.
Jaji amesema kati ya shahidi wa kwanza, tatu na wa nne, hakuna hata mmoja aliyetaja jina au eneo la hospitali ambayo mwathirika wa tukio hilo alihudumiwa.
Kwa mujibu wa shahidi wa pili, Ofisa wa Polisi, E 7049 Koplo Silas, aliieleza Mahakama kuwa Juni 21,2017 mrufani alikiri kwa mdomo kutenda kosa hilo.
Katika utetezi wake mrufani alikana kutenda kosa hilo akidai kuwa akiwa kama msaidizi wa kazi za nyumbani (akichunga mifugo yao), wanandoa hao hawakuwahi kumlipa mishahara yake kwa miaka yote mitatu aliyowafanyia kazi.
Alieleza kuwa wakati wa kukamatwa kwake, alikuwa ameanza kudai malipo yake na katika kulipiza kisasi, kwa nia ya kumnyamazisha na kumnyima mishahara yake shahidi wa kwanza na wa tatu (wazazi wa mtoto huyo), walitengeneza kesi hiyo.
Katika rufaa ya kwanza ya mwaka 2020,Mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo kwa kukosa mashiko ambapo alikuwa na sababu tisa za rufaa.
Katika rufaa ya pili mrufani huyo alikuwa na sababu saba za rufaa ambazo ni Mahakama ya kwanza ya rufaa ilikosea kisheria kushikilia hukumu ya mahakama ya chini, hukumu hiyo ilitokana na ushahidi unaopingana na usioaminika.
Sababu ya tatu ni hukumu hiyo ilitokana na ushahidi wa shahidi wa pili ambaye hakumuhoji mrufani, hukumu hiyo ilitokana na usikilizwaji wa awali ambao haukuhudhuriwa na mrufani, mahakama ya kwanza ya rufaa haikutathmini upya ushahidi na kesi hiyo haikuthibitishwa bila shaka yoyote.
Nyingine ni tofauti ya tarehe ambapo shahidi wa nne alieleza kuwa mtoto huyo alipelekwa kwake Septemba 20,2017 huku ushahidi wake ukiwa tofauti na wa wazazi wa mtoto huyo ambao walieleza kumpeleka mtoto huyo hospitali Juni 20,2017.
Wakati wa kusikilizwa kwa rufaa hiyo, Jumanne alijitetea mwenyewe bila uwakilishi wa wakili huku Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Frdesta Uisso.
Akijibu hoja ya tofauti ya miezi, Wakili Uisso alidai kuwa huo ni upungufu mdogo.
Jaji Galeba amesema katika rufaa ya kwanza, kumbukumbu za rufaa hiyo katika ukurasa wa 66 zinaonyesha kuwa mahakama hiyo ilieleza kuwa tofauti hiyo haiingii kwenye mzizi wa kesi, kwani kielelezo cha kwanza PF3 kinaonyesha kilifunguliwa Juni 20,2017.
Hata hivyo, PF3 ambayo Mahakama ya rufaa ya kwanza ilirejelea, ilifutiliwa mbali na Mahakama hiyohiyo, hali iliyowalazimu Majaji hao wa Mahakama ya Rufani kujadili kisheria kuhusu hati ambayo imefutwa na Mahakama.
Jaji Galeba amesema kisheria, baada ya kufuta hati kutoka kwenye rekodi, Mahakama inazuiwa kuirudia ili kuimarisha ushahidi wa upande ulioitoa.
Kuhusu hoja ya Wakili Uisso kuwa hati inapofutwa, ushahidi mdogo ambao haujaathiriwa hubaki na kuwa hiyo haimaanishi kwa ubora wa ushahidi kabla na baada ya kufutwa kielelezo unabaki vilevile.
“Katika suala hili, katika kesi hii, matokeo mawili yanaonekana, moja, wakati PF3 ilifutwa, ushahidi wa shahidi wa nne ulibaki dhaifu sana kwa sababu pia unakinzana na ule wa shahidi wa kwanza na wa tatu kuhusu tarehe ambayo mtoto alipelekwa hospitali,”amesema.
Jaji huyo amesema kwa sababu hizo mbili, tatizo lingine katika ukurasa wa 25 wa kumbukumbu ya rufaa hiyo wakati wa ushahidi wa msingi, shahidi huyo alieleza kuwa mtoto huyo wa kiume alipelekwa kwa ajili ya uchunguzi na baadaye aligundulika ana michubuko na mbegu za kiume kwenye nguo zake.
Jaji ameeleza kumbukumbu inaonyesha baadaye shahidi huyo alieleza kuwa baba wa mtoto huyo alieleza mtoto wake amelawitiwa na mrufani alidaiwa kukiri akieleza alipitiwa na shetani kutenda kosa hilo.
“Nukuu hizo mbili kuhusu uthibitisho wa kutendeka kosa hilo hauwiani kwa kuwa upande mmoja shahidi anasema alifanya uchunguzi wa kimatibabu, na muda mfupi baadaye alieleza baba wa mtoto huyo ndiye alisema mtoto wake amelawitiwa na mrufani alikiri kutenda kosa hilo.
“Kwa hiyo ni msimamo wetu thabiti kwamba, shahidi wa nne hakuwa shahidi wa kuaminika na si tu ushahidi usioeleweka alioutoa, bali pia utofauti wa maelezo kati ya ushahidi wake na ule wa mashahidi wengine,”
“Hata kama angeaminika, thamani ya ushahidi wake ulipungua pale mahakama ya kwanza ya rufaa ilipofuta PF3. Kwa hivyo, malalamiko katika msingi wa kwanza wa rufaa hayana sifa,”
Baada ya kupitia sababu zote majaji hao walieleza kuwa wanakubaliana na mrufani kwamba ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa tatu na wa nne, haukuwa wa kuaminika kutokana na kutofautiana.
Jaji Galeba amesema kuwa matokeo hayo yanawapeleka kwenye tathmini ya ushahidi pekee uliosalia wa upande wa mashtaka, ambao ni wa shahidi wa pili.
Amesema ushahidi huo una mapungufu mengi ikiwemo kutokutaja jina la mwathirika wa tukio hilo, ushahidi uko kimya juu ya lini na wapi kosa lilitendeka na kuwa hati ya mashitaka ilitaja eneo na tarehe kosa lilipofanyika, ila ushahidi kuwa kosa lilitokea eneo hilo haukutolewa.
Jaji Galeba amesema sheria inaelekeza kukiri kwa mdomo hatia kunakofanywa na mtuhumiwa mbele ya shahidi wa kutegemewa kunaweza kutosha kumtia hatiani.
Jaji Galeba amesema wamepitia kumbukumbu hakuna mahali mahakama zilionyesha jitihada za ziada kujiridhisha kuwa mrufani alikiri kwa hiari, hivyo wanashikilia kuwa ushahidi wa shahidi wa pili haukufikia kiwango kinachohitajika ili kuendeleza hukumu ya mrufani.
Mahakama hiyo ilihitimisha kuwa kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa bila kuacha shaka, hivyo kuamuru aachiwe huru.