
Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini kimemvua uongozi mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Lemburus Mchome leo Jumamosi, Mei 17, 2025.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Ndonde Tottinan amethibitisha kuvuliwa uongozi wa Mchome katika kikao cha mashauriano Mkoa wa Kilimanjaro, kilichoketi leo Mei 17, 2025 mjini Moshi.
Mwananchi limemtafuta Mchome kuhusu taarifa hizo ambapo amedai hana taarifa lakini huenda suala hilo likawa kweli kwa kuwa dalili zilianza kuonekana siku nne zilizopita alipoondolewa kwenye makundi sogozi ya WhatsApp kuanzia la Kanda ya Kaskazini, mkoa hadi wilaya.
Mchome amekutana na kadhia hiyo kipindi ambacho amekuwa na migogoro na chama chake hasa baada ya barua ya malalamiko dhidi ya baadhi ya viongozi wa sekretarieti na kamati kuu akidai walipitiswa na Baraza Kuu Januari 22, 2025 likiwa halina akidi.
Malalamiko hayo ambayo aliyawasilisha ndani ya chama chake na nakala kwa msajili, yamefanyiwa kazi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambapo ameitaka Chadema kuitisha Baraza Kuu jipya ili kufanyia kazi upungufu huo.
Waliopitishwa na Kikao hicho chini ya uenyekiti wa Tundu Lissu wako wanane akiwemo Katibu Mkuu, John Mnyika, naibu makatibu wakuu, Amani Golugwa (Bara), Ally Ibrahim Juma (Zanzibar) na wajumbe wa kamati kuu, Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala ambaye pia aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi