
Dar es Salaam. Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema hoja ya tuhuma za ubadilifu zilizoibuliwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ni cheche za kisiasa, kwani hakuna hata senti moja ya wananchi iliyopotea.
Mchengerwa amezungumza hayo leo Jumanne Aprili 22, 2025 wakati akijibu hoja zilizochangiwa na wabunge wakati wa bajeti ya wizara hiyo.
Amesema atatoa taarifa sahihi kwa muda atakaopangiwa na Spika wa Bunge kuhusu tuhuma za Gambo alizoziibua bungeni hapo Aprili 16, 2025 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo.
Mchengerwa ameonya wabunge wasipende kutumia majukwaa kufanya kiki za kisiasa na kuacha kuhukumu kwa jazba kwani, Tamisemi haitakuwa tayari kuvumilia mambo hayo.
Katika mchango wake Gambo aliibua tuhuma kuwa katika ujenzi wa jengo la utawala na soko jijini Arusha, fedha nyingi zilikuwa zimetumika vibaya akaomba uchunguzi wa kina ufanyike kwenye maeneo hayo.
“Spika, niseme tu maneno ya mwisho katika taarifa hiyo, hakuna senti ya Watanzania iliyopotea kwenye ujenzi huo, tuache cheche za kisiasa, tuhoji kwa hoja na tusihukumu kwa jazba,”amesema Mchengerwa.
Katika hatua nyingine alizungumzia kuwapo upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo 51,262 kwa shule za msingi na sekondari.
Waziri ametaja upungufu huo unasababisha wanafunzi wa kiume kwa shule za sekondari kutumia tundu moja kwa wanafunzi 35 badala ya 25 na wasichana 35 wakitumia tundu moja badala ya 20 kama sera inavyotaka.
Kwa upande wa shule za msingi amesema wanatumia tundu moja wanafunzi 43 wakati mwongozo unataka litumiwe na wanafunzi 25 hivyo Serikali imeamua kutenga Sh26.57 milioni kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 25,880 kwa shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema vifaa vya maabara kwa shule zote 426 zikiwamo 26 za sayansi za wasichana zilizojengwa hivi karibuni, vimeshanunuliwa na kazi iliyopo kwa sasa ni usambazaji.
Kuhusu malipo ya madeni na malimbikizo, amesema Serikali imekuwa ikilipa kutokana na uhakiki ambapo mwaka 2023/24 zililipwa jumla ya Sh116.08 bilioni na mwaka 2024/25 Serikali ililipa Sh78.75 bilioni.
Waziri ameziagiza halmashauri 36 zenye uwezo kuendelea kulipa malimbikizo ya madeni wakati Serikali ikiendelea kuhakiki madeni ya halmashauri zisizo na uwezo ili yalipwe, huku akitoa onyo kwa wahusika wanaoendelea kuzalisha madeni kuacha mara moja.
Amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kutumia nafasi zao kulinda amani na utulivu lakini kuzima migogoro ambayo inaibuka katika maeneo yao, badala ya kusubiri maagizo kutoka ngazi ya juu.