Mchengerwa awaka wanafunzi kukaa chini, aagiza ma-DED, maofisa elimu kujieleza

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amemwagiza katibu mkuu wa wizara hiyo kuwaandikia barua wakurugenzi wa halmashauri na maofisa elimu wa mikoa na wilaya ambako kuna wasio na madarasa.

Mchengerwa amesema ni aibu kwa karne ya sasa kukuta wanafunzi wanasomea chini ya mikorosho wakati kuna baadhi ya wakurugenzi ambao wapo tayari kuhonga Sh20 milioni ili taarifa yake ipite, lakini wanashindwa kutoa fedha za kujenga vyumba vya madarasa ili wanafunzi wasome kwa amani.

Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 13, 2025 kwenye semina ya watumishi wa Tamisemi makao makuu kuhusu jinsi ya kukabiliana na msongo wa mawazo mahali pa kazi, iliyofanyika jijini Dodoma.

“Nimeona jana Nanyumbu au Nanyamba kule Mtwara kuna shule kama nne hivi, watoto wanasoma chini ya mikorosho na kipindi hiki cha mvua watoto wameyageuza madawati yao ili yasilowane mahali wanapokalia, na wameenda kujificha kwenye darasa moja kwa sababu wote wapo kwenye mikorosho, sasa si karne hii na si wakati huu ambao mimi ni Waziri wa Tamisemi,” amesema Mchengerwa.

Ameagiza kukarabatiwa shule za msingi na sekondari ambazo zimejengwa miaka ya 1960 hadi 1970 kwa kuwa malalamiko ni mengi, kuwa zimechakaa.

Baadhi ya watumishi wa ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wakiwa kwenye mafunzo ya kukabiliana na msongo wa mawazo mahali pa kazi leo Februari 13, 2025 jijini Dodoma. Picha na Rachel Chibwete

 “Pesa mlizonazo mzigawanye vizuri ili wale wanaosomea chini ya mikorosho na wanaokaa kwenye sehemu ambayo hakuna madarasa ndiyo muanze kuwajengea madarasa, msimsubiri waziri. Nyinyi mna timu mpaka kule chini, mna wataalamu kule chini, likija jambo ambalo halijaanzia chini mfukuze yule wa chini kwa sababu ameshindwa kusimamia na kuleta taarifa kwa wakati,” amesema Mchengerwa.

“Mimi napokea taarifa kutoka kwa mbunge…na mkurugenzi wa elimu hujui kama kuna watu wanakaa kwenye mikorosho maana yake ni nini, yule msaidizi wako hakufanya kazi vizuri kukuletea taarifa ili tukatafute hizo fedha watoto wetu wakae wasome sehemu nzuri. Sasa kama taarifa inakuja huku juu, ina maana yule kule chini mfukuze, kesho umwondoe arudi kufundisha nafasi aliyonayo atoke.”

Amesema haiingii akilini watoto wakae kwenye mikorosho na wakati ofisa elimu yupo pamoja na mkurugenzi wa halmashauri, ambao wanashindwa kutumia hata makusanyo yao ya ndani kujengea madarasa.

“Mkurugenzi wa halmashauri anafanya kazi gani anakosa mapato ya kujenga hata darasa moja au mawili, lakini wakati mwingine wanakuwa na fedha za kwenda kuhonga watu, yaani mtu anaona atoe Sh20 milioni akahonge ili taarifa yake ipite, lakini hawezi kupeleka hiyo fedha kujenga darasa,” amesema Mchengerwa.

Amewataka watumie fedha zilizotengwa kwa ajili ya maboresho kufanya ukaguzi nchi nzima kujua maeneo gani ambako watoto wanakaa chini ya mikorosho ili waweze kujengewa hata darasa moja badala ya kuwaacha wakinyeshewa na mvua.

Amemwagiza katibu mkuu kumwaandikia mkurugenzi wa elimu Tamisemi kufanya tathmini ya nchi nzima ili kujua maeneo ambayo watoto wanakaa chini ya mikorosho na kuwaandikia wakurugenzi waje watoe maelezo yao pamoja na wataalam na wasaidizi wao, ni kwa nini wasichukulie hatua dhidi yao.

Amesema pamoja na hao, maofisa elimu wa mikoa na wilaya kama hawakuleta taarifa na wataalamu wengine wanaohusika na hili, wachukuliwe hatua.

Amesema kwenye sekta ya elimu kupitia miradi ya Boost na Sequip, Tamisemi imetenga fedha nyingi za kujenga shule mpya na kutaka maeneo ambayo watoto wanakaa chini yapewe kipaumbele cha kujengewa shule mpya au kuongezewa madarasa, akisisitiza kwa mwaka wa fedha uliopo kuna Sh1 trilion kwa ajili ya elimu.

Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, Sospeter Mtwale amesema mafunzo hayo ni maalumu kwa ajili ya kuwafanya watumishi wa ofisi hiyo kukabiliana na msongo wa mawazo wanapokuwa kazini.

Amesema wanatumia muda mwingi kazini hivyo kama hakutakuwa na mahusiano mazuri kwenye utendaji wao, wanaweza kupata changamoto ya afya ya akili inayotokana na kazi.

Walichokisema wasomi

Akizungumzia suala la wanafunzi kukosa madarasa, Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Dk Ombeni Msuya amesema watendaji husika wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kushindwa kusimamia maendeleo ya elimu kwenye maeneo yao.

Amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwenye sekta ya elimu zaidi ya Sh15 trilioni kwa ajili ya kujenga shule mpya na madarasa kwenye maeneo ambayo hayana ya kutosha, hivyo kama bado kuna changamoto za wanafunzi kusoma chini ya mikorosho, watendaji wanapaswa kuchukuliwa hatua.

“Nitashangaa kama mpaka sasa kuna wanafunzi wanaosomea chini ya mikorosho halafu wakurugenzi hawajachukuliwa hatua zozote,” amesema Dk Msuya.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma, Dk Erasto Kano amesema kuwa Serikali imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya elimu, hivyo watoto kuendelea kusomea chini ya mikorosho inadhihirisha kuwa kuna baadhi ya watendaji ambao hawatimizi wajibu wao.

Amesema mwaka huu hazijasikika taarifa za wanafunzi kushindwa kwenda shule kwa kukosa madarasa, hali inayoonyesha kuwa Serikali imejipanga vizuri kuwahudumia wanafunzi wote waliodahiliwa au kuchaguliwa kujiunga na elimu ya msingi au sekondari.

“Hii ni aibu kwa taifa kubwa kama Tanzania halafu wanafunzi wanaendelea kusomea chini ya miti…siyo tu kwa sababu ya kipindi cha mvua hata kama kungekuwa hakuna mvua, hii ni aibu kwa taifa, wanaohusika na kusimamia elimu kwenye maeneo hayo wachukuliwe hatua kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao,” amesema Dk Kano