Mchengerwa ataja vipaumbele sita maboresho Dart

Dar es Salaam. Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart), katika mwaka wa fedha 2025/26, unatarajiwa kukamilisha ununuzi wa mtoa huduma kwa njia ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika awamu ya pili ya mradi huo.

Sambamba na hilo, wakala huo maarufu ‘mradi wa mwendokasi’ unatarajia kukamilisha ufungamanishaji wa mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji nauli na wa kuongoza magari.

Mambo hayo ni kati ya sita yanayotarajiwa kutekelezwa na Dart inayohitaji bajeti ya Sh4.83 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kati ya hizo Sh4.10 bilioni mishahara na Sh731.21 milioni matumizi mengineyo.

Hayo yameelezwa leo, Jumatano Aprili 15, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26 ya Sh11.7 trilioni.

Amesema katika kipindi hicho, Dart itakamilisha taratibu za ununuzi wa mtoa huduma kwa njia ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi wa awamu ya kwanza na ya pili.

Lingine, amesema wakala huo, utaendelea na maandalizi ya usanifu na ujenzi wa miundombinu ya awamu ya tano ya Barabara za Nelson Mandela, Mbagala, Tabata -Segerea – Kigogo zenye urefu wa kilomita 26.

“Kuendelea na ukarabati wa mara kwa mara wa miundombinu ya mfumo wa mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa vituo vya mchepuko,” amesema Mchengerwa.

Mchengerwa amesema wakala huo utakamilisha ufungamanishaji wa mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji nauli na ule wa kuongozea magari, ikiwa ni sehemu ya maboresho endelevu ya huduma hiyo kwa wananchi wa Dar es Salaam.

Wakala huo pia kwa mujibu wa Mchengerwa, utafanya pembuzi yakinifu nne kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu ya barabara za nyongeza za BRT Rangitatu – Vikindu kilomita tano, Tegeta – Bunju kilomita 13, Kimara – Kibaha kilomita 20 na kuunganisha BRT awamu ya kwanza na nne kupitia Barabara ya Mwai Kibaki kilomita saba.

“Pia itafanya utafiti na kuibua vyanzo vipya vya mapato ya ndani kwa kuendeleza maeneo ya ushoroba wa mradi, ikiwemo ujenzi wa vitega uchumi kwenye maeneo ya Mtoni kwa Aziz Ally na eneo la Kariakoo Gerezani,” amesema.

Katika maelezo yake, Mchengerwa amesema kwa muda mrefu watu wa Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakisubiri, wengine kwa matumaini na wengine kwa mashaka lakini wote kwa kiu ya mabadiliko.

“Leo, kwa mara ya kwanza tunasema, subira yao haikuwa ya bure. Kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP), tumefanikisha hatua ya kihistoria kusaini mikataba na watoa huduma watatu wa uendeshaji wa awamu ya pili ya mabasi yaendayo haraka. Hili ni tukio la mwanzo wa zama mpya  siyo tena hadithi ya ahadi zisizotekelezwa, bali ya huduma bora zinazoonekana na kuguswa,” amesema Mchengerwa.

Waziri huyo amesema wanafalsafa wanasema, ‘Mambo Makubwa Yanahitaji Muda’. Hatua hii si tu ununuzi wa huduma, bali ni ununuzi wa matumaini mapya kwa wakazi wa jiji letu. Hatutaki kurudia makosa ya jana, bali tunajenga mfumo imara, unaozingatia ubora, ufanisi na heshima kwa muda na maisha ya abiria.

“Kwa miaka mingi wananchi wamepitia usumbufu, foleni zisizokwisha na huduma zisizoeleweka. Lakini leo, tunasema kwa sauti ya matumaini: nuru inaanza kuonekana. Mabasi haya hayatakuwa tu magari ya kusafirisha watu , yatakuwa magari ya kusukuma uchumi, kuunganisha fursa na kupunguza mzigo wa maisha ya kila siku,” amesema.

Mradi wa BRT unaotoa huduma kwa sasa ni awamu ya kwanza, inayohusisha barabara ya Morogoro kutoka Mbezi-Kimara-Kivukoni. Pia, Kimara-Morocco na Kimara-Gerezani.

Awamu hiyo imegubikwa na malalamiko kutoka kwa wananchi, kutokana na uchache wa mabasi unaosababisha abiria kukaa muda mrefu vituoni bila huduma, huku mabasi yakijaza na kupitiliza.

Hata hivyo, Serikali imetangaza kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha, itapokea mabasi 77 kwa ajili ya kutoa huduma katika mradi huo, na la mfano, litawasili Mei.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *