Mchengerwa ataja vipaumbele bajeti ya Tamisemi 2025/26

Dar es Salaam. Udhibiti wa matumizi yasiyo na tija ni miongoni mwa vipaumbele vinavyojirudia katika bajeti za Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) 2025/26 huku kukiwa na mapengo ya utekelezwaji wake.

Mapengo hayo yanathibitishwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), katika mwaka unaoishia Machi 2024.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mamlaka 26 za serikali za mitaa zilielekeza Sh7.73 bilioni katika kutekeleza miradi na matumizi ya kawaida ambayo hayakuwa sehemu ya mpango uliokusudiwa awali.

Kama hiyo haitoshi, ripoti hiyo imebaini matumizi yasiyokuwa na tija ya Sh224.46 bilioni yaliyobainika katika mamlaka za serikali za mitaa, Serikali Kuu na taasisi za umma.

Kipaumbele hicho kimetajwa bungeni jijini Dodoma leo, Jumatano Aprili 16, 2025 na Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa ikiwa ni sehemu ya wasilisho lake la makadirio ya bajeti ya Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2025/26 ya Sh11.78 trilioni.

Amesema Sh7.83 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh6.26 trilioni kwa ajili ya matumizi mengineyo. Amesema Sh1.5 trilioni, ikijumuisha Sh1.06 trilioni za mapato ya ndani ya halmashauri.

Katika hotuba yake, amesema Tamisemi katika mwaka huo wa fedha, itaratibu na kusimamia mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi yasiyo na tija katika ngazi zote.

Wakati Tamisemi ikiweka kipaumbele hicho, kumeonekana kasoro katika utekelezaji kama inavyoshuhudiwa katika ripoti ya CAG.

“Nimebaini mamlaka 26 za Serikali za Mitaa zilielekeza Sh7.73 bilioni katika kutekeleza miradi na matumizi ya kawaida ambayo hayakuwa sehemu ya mpango uliokusudiwa awali,” amesema.

Mbali na hilo, vipaumbele vingine vinavyotekelezwa kwa bajeti hiyo, amesema ni kusimamia shughuli za utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na ugatuaji wa madaraka kwa umma.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, katika mwaka huo wanatarajia kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa huduma za jamii.

Vingine, amevitaja ni ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi zinazosimamiwa na ofisi hiyo.

Pia, ametaja uratibu wa usimamizi wa mifumo ya Tehama, kuendeleza rasilimali watu katika ngazi zote za Tamisemi na kuratibu na kusimamia shughuli za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wa wizara hiyo mikoa na mitaa.

Mchengerwa ametaja kuratibu na kushiriki michezo ya shule za msingi Umitashumta, sekondari Umisseta na mashindano ya michezo ya shule za sekondari za Afrika Mashariki.

Vipaumbele vingine ni kuratibu shughuli za utendaji wa kazi wa taasisi zilizopo chini ya Tamisemi, kadhalika kuratibu na kusimamia ujenzi wa miradi ya maendeleo katika ngazi zote za wizara hiyo.

Ametaja kuratibu uibuaji wa miradi ya kimkakati na inayopaswa kutekelezwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika mamlaka za serikali za mitaa.

Amesema wizara hiyo itasimamia na kuratibu shughuli za utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa maliasili katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, kipaumbele kingine ni kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za mabadiliko ya tabianchi na uendelezaji wa utalii, uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia na uendelezaji wa biashara ya kaboni katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.

Kipaumbele kingine, amesema ni kuratibu shughuli za uendelezaji wa vijiji na miji kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *