Dar es Salaam. Mikakati ya Serikali katika kuwainua wachimbaji wadogo, ujenzi wa minada ya kimataifa ya vito na udhibiti utoroshwaji wa madini ni miongoni mwa mambo yaliyoiwezesha sekta ya madini kukua kwa kasi nchini Tanzania.
Hatua hiyo imekuwa kichocheo na kuifanya sekta ya madini kuvuka lengo lake la kuchangia asilimia 10 katika Pato la Taifa ifikapo mwaka 2026.
Hata hivyo, leo Aprili 23, 2025 akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kuwa sekta ya madini imepiga hatua kubwa na ya kihistoria kwa mchango wake kufikia asilimia 10.1 kwenye pato la Taifa mwaka 2024.

Amesema lengo lililowekwa kwenye Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026 ni kuwa sekta hiyo ifikie asilimia 10 kwenye pato la Taifa.
“Ni jambo la kujivunia kuona kuwa juhudi za Serikali na wadau wa sekta hii zimezaa matunda. Mwaka 2023 tulikuwa na mchango wa asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa. Leo hii, tunazungumza kuhusu ongezeko hadi asilimia 10.1 kwa mwaka 2024.
Hili si jambo dogo. Haya yote yamefanikiwa kutokana na usimamizi na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutokana na msukumo mkubwa ambao amekuwa akiuweka.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
Kuna maboresho mengi yamefanyika kuhakikisha tija kwa wachimbaji wadogo na wadau wote wa madini inapatikana,” amesema Mavunde.
Amesema kwa miaka minne kumefanyika mabadiliko makubwa ya kimfumo na kisheria katika sekta ya madini nchini na kwamba, ukuaji huo ni matokeo chanya na yenye tija kwa sekta nzima.
Amezitaja hatua kadhaa zilizochangia mafanikio hayo kuwa ni kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli ya Serikali kupitia sekta hiyo, kuanzishwa kwa minada ya madini ya vito, udhibiti wa utoroshwaji wa madini.
Pia, kuanzishwa kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini, pamoja na kuanza kwa ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Waziri Mavunde ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wadau katika sekta ya madini nchini wakiwemo wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo na mnyororo mzima wa sekta hiyo kuendelea kuchapa kazi kwa bidi kwa kuwa, uboreshwaji wa mazingira utaendelea kuzingatiwa.
Pia, ameagiza wawekezaji kuendelea kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa chini ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, huku wizara ikiendelea kutoa ushirikiano kwa wote wenye nia ya kuwekeza kwa tija.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mafanikio hayo yameonesha wazi kuwa sekta ya madini si tu kichocheo cha ukuaji wa uchumi bali pia ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni, ajira na maendeleo ya kijamii kwa Watanzania.