
Dodoma. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Nchini (NHIF) umeanza mkakati wa kuwafikia Watanzania maskini wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu ili kuwasaidia kwa kiwango cha chini.
Mpango huo ni utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote katika kifungu cha 25, na hivyo mpango huo unatarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa ukiwashirikisha Ofisi ya Rais Tamisemi na Mpango wa Kuhudumia Kaya Masikini (Tasaf).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Machi 10, 2025, Mkurugenzi wa NHIF, Dk Irene Isaka, amesema utekelezaji wa mpango huo utazisaidia kaya maskini ambazo zitaainishwa kupitia mamlaka za Serikali za mitaa kwa nchi nzima.
“Huu ni mkakati maalumu ambao tumeuanzisha mchakato wake, mapema tutaanza kupitia katika maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na wenzetu Tamisemi, Tasaf, na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ili tuwabaini watu katika kaya za wasiojiweza, tuwakatie tuwape ahueni hiyo,” amesema Dk Irene.
Hata hivyo, Oktoba 23, 2024, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, alisema kaya maskini zipatazo milioni 1.2 nchini zitanufaika na mpango wa Serikali wa kusaidia kaya zisizojiweza ili zipate huduma za afya kupitia Bima ya Afya kwa Wote.
Leo, Dk Irene amesisitiza kuwa jambo hilo limepewa kipaumbele, kwani afya ya mwanadamu ndiyo msingi na kwamba wametambua wapo watu ambao hawawezi kumudu gharama za matibabu, licha ya uhitaji walionao.
Kwa mujibu wa NHIF, hadi sasa ni asilimia nane tu ya Watanzania ndiyo wanahudumiwa na mfuko huo katika vituo 10,004, jambo alilosema bado kunahitajika elimu ya kutosha ili kuondoa imani za kuwa watu wanalipia fedha zao lakini hawaugui.
Akizungumzia ongezeko la wanachama, amesema katika kipindi cha miaka mitatu wamesajili zaidi ya wanachama milioni 2.2 na kukusanya Sh2.3 trilioni.
Kwa mujibu wa Dk Irene, katika kipindi hicho wamelipa Sh2.29 trilioni kwa vituo vya afya na hospitali zilizotoa huduma kwa wateja wao, huku Sh91 bilioni kati ya hizo zilitumika kulipia huduma za watumishi wastaafu waliokuwa wanachama wa mfuko huo kabla ya kustaafu kwao.
“Lakini, niseme kuwa katika fedha tulizolipa, asilimia 60 ilikuwa malipo yaliyotokana na tiba za magonjwa yasiyoambukiza, lakini tulifanikiwa kudhibiti upotevu wa mapato kwa kuokoa Sh22 bilioni ambapo kadi 13,000 tulizifungia na watumishi 36 walikuwa kwenye hatua ambapo zaidi ya 15 tuliwasimamisha na wengine majalada yao yapo katika hatua mbalimbali,” anasema.
Kuhusu uwezo wa mfuko huo, amesema hivi sasa wanaweza kutoa huduma kwa miezi 14 kutoka uwezo wa miezi sita waliokuwa nao, huku wakijivunia kuondoa hasara iliyokuwepo ya Sh120 bilioni hadi sasa wana uwezo wa ziada ya Sh95 bilioni.
Tamko la Wizara ya Afya
Oktoba 23, 2024, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, alisema kaya maskini zipatazo milioni 1.2 nchini zitafikiwa na mpango huo.
Waziri Mhagama alisema Tanzania Bara ina jumla ya kaya 14.8 milioni, ambapo kaya milioni 3.9 ni kaya zisizo na uwezo. Kati ya kaya hizo zisizo na uwezo, kaya milioni 1.2 Sawa na asilimia 32.3, Serikali imejipanga kuanza ugharimiaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kundi hilo ambalo linatambuliwa kama kaya zenye umaskini uliokithiri zinazotambuliwa na (TAsaf), unaohusika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
“Kifungu cha 25 cha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Sura Namba 161, kimeanzisha Mfuko wa Kugharamia Bima ya Afya kwa Watu Wasio na Uwezo, ambapo Serikali imejipanga kuanza ugharamiaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kaya Milioni 1.2 ambazo zinatambuliwa kama kaya zenye umaskini uliokithiri,” amesema Waziri Mhagama.