Mchakamchaka urais 2025 ndani ya vyama pamoto

Dar es Salaam. Wakati mchakato wa kuwapata wagombea urais wa Tanzania Bara na Tanzania ukiendelea kushika kasi kwenye vyama vinne vya siasa, vyama vingine pia viko mbioni kuanza mchakato huo.

Pazia la kuwapata wagombea urais ndani ya vyama lilifunguliwa Januari 2025 na Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichowapitisha Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais, huku mgombea mwenza akiwa Dk Emmanuel Nchimbi.

Pia, chama hicho tawala kilimpitisha Dk Hussein Mwinyi, kuwa mgombea urais wa Zanzibar.  Wakati Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud akichukua na kurejesha fomu ya kuwania urais wa visiwa hivyo, akitarajiwa kuchuana na Dk Mwinyi anayetetea nafasi hiyo.

Vyama vingine vilivyoanza mchakato huo ni NLD ambapo katibu mkuu wa chama hicho, Hassan Doyo alichukua fomu na kutaja vipaumbele 10 atakavyovitekeleza endapo akifanikiwa kuibuka kidedea.

Mbali na Doyo, yupo Innocent Siriwa, Naibu Katibu wa ADC (Bara), amechukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania urais, akisema endapo atashinda nafasi hiyo, atahakikisha anapigania upatikanaji wa Katiba mpya, elimu bora na Afya.

Machi 29, 2029, NCCR Mageuzi nacho kilimpitisha, Haji Ambari Khamis kuwa mgombea urais wa Tanzania, huku mgombea mwenza akiwa Joseph Selasini ambaye ni mbunge wa zamani wa Rombo mkoani Kilimanjaro.

Wakati huohuo, Katibu wa AAFP, Rashid Rai amesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu umeanza tangu Aprili 15, 2025 ukitarajiwa kukamilika Aprili 22, ingawa bado makada hawajajitokeza.

“Mkutano mkuu wa chama utafanyika Aprili 29 kwa ajili ya kupitisha majina ya wagombea urais, naamini hadi muda watakuwa wameshajitokeza, kama ilivyoanza Zanzibar ambapo mwenyekiti wetu, Said Soud ameonyesha nia ya kuutaka urais,” amesema Rai.

Wakati vyama hivyo vikiwa mguu sawa kuwapata wagombea wao, vyama vingine vya CUF, AAFP, Ada Tadea, DP na Chaumma, viko mbioni kuanza mchakato huo ili kuwapata wagombea watakaopeperusha bendera za vyama vyao.

Akizungumza na Mwananchi Digital Alhamisi, Aprili 17, 2025 Katibu Mkuu wa CUF, Husna Mohamed Abdallah amesema wakati wowote wanaanza mchakato wa utoaji wa urejeshaji wa fomu kwa ngazi ya urais wa Tanzania na Zanzibar.

“Tulikuwa tunasubiri mfungo wa Ramadhan kukamilika, tupo katika majadiliano, wakati wowote tutaanza kutoa fomu hizo, tayari kuna makada kadhaa wameonyesha nia ya kuutaka urais Tanzania na Zanzibar,” amesema

“Inawezekana kabla ya Aprili kuisha tukaanza mchakato huu, tunataka idadi ya wanaonyesha nia iongezeke zaidi. Tumefungua milango kote Zanzibar na Tanzania, naamini watajitokeza zaidi,” amesema Abdallah

Mwenyekiti wa Ada Tadea, Juma Ali Khatib amesema ameshaweka wazi kwamba atawania urais wa Zanzibar baada ya pazi la kuchukua na kurejesha fomu kufunguliwa.

“Tunatarajia Mei mwanzoni kufanya mkutano mkuu wa chama kwa ajili ya kupitisha majina ya wagombea wa urais,” amesema Khatib ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa.

Katibu wa AAFP, Rashid Rai amesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu umeanza tangu Aprili 15, 2025 ukitarajiwa kukamilika Aprili 22, ingawa bado makada hawajajitokeza.

“Mkutano mkuu wa chama utafanyika Aprili 29 kwa ajili ya kupitisha majina ya wagombea urais, naamini hadi muda watakuwa wameshajitokeza, kama ilivyoanza Zanzibar ambapo mwenyekiti wetu, Said Soud ameonyesha nia ya kuutaka urais,” amesema Rai.

DP, Chaumma bado bado

Wakati vikionyesha utayari wa kuwapata wagombea vyama vya Chaumma na Democratic Party vimesema bado bado huku vikisikilizia mchakato huo.

“Bado hatujapanga wala kufikiria tunaanza lini,” amesema Rungwe maarufu ‘Mzee wa ubwabwa’.

Wakati Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema wanafikiria kuanza mchakato huo ifikapo Juni Mosi mwaka huu, kwa kuanza kutoa fomu za urais wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *