Mbunge wa chama cha Leba nchini Uingereza Zarah Sultana amekosoa vikali mashirikisho ya juu ya soka duniani ya FIFA na UEFA kwa kutoziadhibu timu za soka za Israel wakati utawala huo wa Kizayuni unaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
Sultana amekumbusha kuwa Russia ilipigwa marufuku haraka kushiriki mashindano yote ya UEFA na FIFA baada ya kuanzisha vita dhidi ya Ukraine mwaka 2022.
Lakini mkabala wake, Israel haijawekewa vikwazo kama hivyo baada ya kupita miezi 13 ya mauaji ya kimbari unayoendeleza huko Ghaza.
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X, mbunge huyo wa chama cha Leba nchini Uingereza amesema, hali hiyo inadhihirisha “vigezo vya kiundumakuwili vya ubaguzi wa rangi vilivyojikita katika sera za kimataifa na michezo”.
Mashirikisho ya juu ya usimamizi wa michezo duniani yamekosolewa na wengi kwa kuruhusu timu na wanariadha wa Israel kushiriki mashindano ya kimataifa ya michezo ilhali FIFA kwa upande wa soka, FIBA katika mpira wa vikapu, na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki zilichukua hatua za kuipiga marufuku Russia bila kupoteza muda.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ungali unaendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ghaza uliyoanzisha Oktoba 7, 2023, licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa vita mara moja.
Wapalestina wapatao 43,700 wameshauawa shahidi huko Ghaza hadi sasa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine zaidi ya 103,000 wamejeruhiwa.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unakabiliwa pia na kesi ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kutokana na vita ulivyoanzisha dhidi ya Ghaza…/