
Nairobi. Mbunge wa Malava katika Kaunti ya Kakamega, Kenya, Moses Injendi amefariki dunia wakati akipatiwa na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.
Hayo yamethibitishwa na Spika wa Bunge Moses Wetang’ula jana Jumatatu Februari 17, 2025 bungeni
“Waheshimiwa wabunge kwa huzuni ninawaarifu kuhusu kifo cha mwenzetu mheshimiwa Moses Malulu Injendi ambaye alituacha leo jioni (jana) Februari 17, 2025 saa kumi na moja na nusu jioni katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi,” amesema.
Injendi, ambaye alikuwa akihudumu muhula wake wa tatu bungeni, alikuwa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu.
Aidha, Wetang’ula amemtaja Injendi kama mbunge aliyewakilisha watu wa eneo bunge lake kwa moyo wa kujitolea na uadilifu wa hali ya juu.
“Michango yake katika michakato ya utungaji sheria haswa sekta ya Elimu na kilimo cha miwa, na uliolenga kuimarisha maisha ya Wakenya, itakoswa,” ameeleza.
Injendi alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge katika uchaguzi mkuu wa 2013 kwa tiketi ya Chama cha Amani National Congress (ANC).
Hata hivyo, alirejea tena bungeni kwa mara ya pili baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 kwa tiketi ya chama cha ODM.
Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Injendi alirejea bungeni kwa muhula wa tatu kwa tiketi ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).
Itakumbukwa Januari 2025, kulisambaa taarifa za uvumi kuhusu kifo chake, lakini ofisi yake ilikanusha madai hayo, ikieleza kuwa alikuwa amelazwa hospitalini kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.
Vilevile, Injendi atakumbukwa kwa michango yake kwa jamii kama vile kuwalipia ada wanafunzi wenye uhitaji katika eneo lake pamoja na kusaidia jamii kupitia Malulu Injendi Foundation iliyoanzishwa kwa lengo la kuboresha maisha ya watu.
Imeandikwa na Evagrey Vitalis kwa msaada wa mashirika.