Mbunge: Dabi ya Karikoo iitwe Samia Dabi

Dodoma. Mbunge wa Busega, Simon Lusengekile ametaka mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Simba maarufu kama Kariakoo Dabi iliyopangwa kupigwa Juni 15, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam kuitwa “Samia Dabi”.

Lusengekile ametoa ombi hilo leo Alhamisi Mei 15, 2025, wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/26, iliyowasilishwa na Waziri Profesa Makame Mbarawa bungeni jijini Dodoma.

“La mwisho mheshimiwa mwenyekiti ni kwamba nimemuona hapa Kaimu Waziri Mkuu Mheshimiwa Mkuchika (Kapt. George Mkuchika-anayekaimu nafasi ya Waziri Mkuu bungeni), ninaomba msimamizi wa shughuli za serikali hapa bungeni siku ya tarehe 15, 6, 2025 Dabi ya Simba na Yanga tuiite jina la Samia Dabi Kampeni,” amesema mbunge huyo.

Awali dabi hiyo ilikuwa imepangwa kufanyika Machi 8, 2025 lakini muda mchache kabla ya mchezo huo, Bodi ya Ligi Kuu Bara iliahirisha mchezo huo kwa madai kuwa Simba ilizuiwa na wanaodaiwa kuwa makomandoo wa Yanga siku moja kabla ya mchezo huo wasifanye mazoezi ya mwisho.

Hata hivyo, Yanga ilienda uwanjani siku hiyo na inashikilia msimamo kuwa haitacheza mchezo ujao wa dabi kwa kuwa wanaamini Bodi iilivunja kanuni kabla ya kuahirisha mchezo wa kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *