Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba amesema kauli zinazotolewa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu kuzuia uchaguzi, ni dalili za kushindwa sawa na watu walioweka mpira kwapani.
Makamba amesema hayo leo Alhamisi Aprili 10, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya Waziri Mkuu ya makadilio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Hatuba hiyo iliwasilishwa jana Jumatano, Aprili 19, 2025 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Wabunge wataijadili kwa siku tano hadi Aprili 15, 2025 ambapo wataipigia kura ya kuipitisha ama kutoipitisha.
Makamba ni miongoni mwa wabunge 19 wa Chadema ambao wamekuwa na mgogoro ndani ya chama chao baada ya kudaiwa kuwa walijipeleka na kula kiapo bila ruhusa ya chama hicho.
Chadema ilitangaza kuwavua uanachama. Wabunge hao akiwemo Halima Mdee walifungua kesi mahakamani ya kupiga kufukuzwa. Tangu kufukuzwa kwao, Chadema imekuwa ikisema haiwatambui.
Chadema inatekeleza azimio lililopitishwa na mkutano mkuu wa Januari 21, 2025 la No reforms, No election (Bila mabadiliko, Hakuna uchaguzi) ambapo viongozi wa kitaifa akiwemo Tundu Lissu wamekuwa wakifanya mikutano ya kuelimisha wananchi.
Mikutano hiyo imefanyika Kanda ya Nyasa na Kusini yenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Hata hivyo, wakati Lissu na wenzake wakiendelea na operesheni hiyo, kumeibuka kundi G55 la watia nia ubunge wa mwaka 2020 na 2025 likijumuisha baadhi ya vigogo wanaokubaliana kwamba No Reforms, lakini siyo kuzuia uchaguzi wakisema kwa mazingira ya sasa jambo hilo haliwezekani.
Wakati Chadema ikiwa na msimamo wa No Reforms, No Election G55 imepinga hatua hiyo jambo ambalo viongozi wakuu wa chama wakiwatafsiri ni wasaliti na wanaokwenda kinyume na uamuzi wa chama hicho.
Kutokana na upinzani huo, baadhi wenyeviti wa kanda wameanza kuwaandika barua wakitakiwa kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua saini zao kuonekana katika waraka wa G55 wenye hoja tisa za kuitaka Chadema ishiriki uchaguzi huku ukiwa na kichwa cha habari ‘ushauri kwa chama’.
Hata hivyo, G55 wanatafsiri hatua ya kuwataka kujieleza ni kama ubepari ndani ya Chadema na kwamba kuwa na maoni mbadala hakupaswi kuonekana kama wasaliti au uadui.
Alichokisema Makamba
Makamba akichangia bajeti hiyo, huku akishangiliwa na wabunge wakiwemo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amesema hakuna mwenye uwezo wa kuuzuia uchaguzi na kwamba anaungana na wanachama 55 wa Chadema waliosema lazima uchaguzi ufanyike.
Makamba ambaye kitaaluma ni mwanasheria amesema kuzuia uchaguzi kwa njia hiyo ni uhaini na jambo hilo halikubariki hivyo akamuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa na vikosi vyake kusimama imara na kutekeleza wajibu wao.
“Wamegundua hawawezi kushinda ndiyo maana wameweka mpira kwapani, hatuwezi kuhamasisha uasi kwenye masuala ya uchaguzi, lazima tushiriki na mimi nitagombea na nitarudi hapa ndani,” amesema Makamba bila kutaja chama kipi atakachopitia.
Amesema malengo ya chama chochote cha upinzani duniani ni kushika dola, hivyo kama watu wanataka kukimbia uchaguzi inaonyesha hawataki kushika dola na hivyo siyo chama hicho.
Mbunge huyu ambaye mwaka 2020 aligombea ubunge Shinyanga Mjini kwa Chadema, amesema yeye hana mahali pa kukimbilia na kwamba pasipoti ya kusafiria aliipata akiwa bungeni hivyo asingetamani kuona yeye na wazazi wake na ndugu zake wakipata misukosuko.
Akizungumzia uchaguzi amesema tangu mfumo wa vyama vingi chama kilichokuwa madarakani ni CCM, lakini wapinzani wamekuwa wakishinda uchaguzi na kutangazwa na ndiyo maana wako ndani ya Bunge.
Kwa mujibu wa Makamba, ni mwaka jana (2024) ambapo Tanzania ilishuhudia mabadiliko na kupata Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo anaamini itakwenda kutenda haki hivyo lazima uchaguzi ufanyike.
“Tumeona bajeti yako Waziri Mkuu mmeongeza fedha kwa ajili ya uchaguzi, mimi nasubiri maboksi ya kura na uchaguzi ufanyike na kura zihesabiwe siyo kususia,” amesema Makamba.
Katika hatua nyingine mbunge huyo amemwagia sifa Rais Samia Suluhu Hassan akisema lazima atapewa mitano mingine kutokana na kazi nzuri aliyoifanya ya kupeleka maendeleo kwa wananchi.
Mara baada ya kumaliza kuchangia, baadhi ya wabunge wenzake wale 19, walinyanyuka na kwenda kumpongeza huku wengine wakimpa fedha ishara ya zawadi.
Mbali na Makamba, wengine kwenye kundi hilo ambao walikuwa na vyeo mbalimbali walivyokuwa wakishikilia katika Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho.
Wabunge hao ni Halima Mdee ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Bawacha, Grace Tendega (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Bawacha) na Esther Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart na Nustrat Hanje (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Bavicha.
Wengine walioingia katika misukosuko hiyo ni Jesca Kishoa (aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha Bara), Hawa Mwaifunga (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bawacha Bara) na Tunza Malapo.
Wengine ni Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest na Conchesta Rwamlaza.
Mchango wa Aida
Akichangia, Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani ametaka Serikali kuweka hadharani sababu za kukamatwa kwa Lissu ili Watanzania wafahamu na haki itendeke.
Lakini akiendelea kuchangia, Mbunge wa Nyasa (CCM), Stella Manyanya alisimama na kutoa taarifa kwa Kenani kuwa angekuwa yeye asingedhubutu kusimama na kumsemea kiongozi wake asiye na heshima.
“Nisingethubutu, kiongozi huyo unayemuita kwamba huyo ni kiongozi mimi nimemshangaa badala kuongea mambo ya msingi amepeleka matusi na kudharau wananchi wa Nyasa kwa kuwasemea viongozi wao, akome akome,” amesema.
Akijibu taarifa hiyo, Khenani amesema:“Nimuombe tu mama yangu, mimi nimelelewa na nimefundishwa yule ni mama yangu na amekuwa mkuu wangu wa Mkoa wa Rukwa ni wajibu wangu kama mbunge na nimesimama kuiambia Serikali haki itatendeka na historia ya nchi yetu iendelee kujengwa ya amani na utulivu.”
Ametaka kama kuna kosa limetendeka basi ielezwe kosa alilolifanya na sababu za kukamatwa.
Lissu alikamatwa jana jioni Jumatano na Polisi Mkoa wa Ruvuma, baada ya kumaliza kufanya mkutano wa hadhara wa No reforms, No election, wilayani Mbinga. Mpaka sasa polisi haijaweka wazi sababu za kumshikilia kiongozi huyo wa upinzani.