Mbunge ataka waliohudumu muda mrefu kamati wapewa ‘CPA’ za heshima

Dodoma. Serikali inaandaa utaratibu wa kuwalipia wabunge gharama za kushiriki kwenye mikutano ya kitaalumu, Bunge limeelezwa, huku mbunge mwingine akitaka kuwa na utaratibu wa kuwapa ‘CPA’ (Certified Public Accountant) za heshima.

Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 14, 2025 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kilindi (CCM), Omari Kigua ambaye ameuliza lini wabunge wenye sifa ya CPA ushiriki wao kwenye Kamati za LAAC, PIC, PAC na Bajeti utachukuliwa kama masaa ya kujifunza.

Waziri amesema kuwa Mwongozo wa Mafunzo endelevu ya Kihasibu Tanzania (Continued Professional Development- CPD Guideline), uliidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA na kuanza kutumika rasmi Julai 01, 2020.

“Mwongozo unatambua mafunzo endelevu rasmi (yaani uso kwa uso, au ya kielektroniki) na mafunzo endelevu yasio rasmi ikiwa ni pamoja na kushiriki mikutano ya kiufundi katika tasnia ya Uhasibu na Ukaguzi,” amesema Dk Mwigulu.

Amesema kwa kufuata mwongozo huo, na kwa kuzingatia muda unaotumiwa na  wabunge wakati wa ushiriki wa mikutano ya kamati za bunge, na hasa zile zinazohusu masuala ya uhasibu au ukaguzi kama LAAC, PIC, PAC na uchambuzi wa Bajeti ya Serikali, masaa wanayotumia wabunge wenye CPA yanatambuliwa kama ni mafunzo endelevu “CPD hours,”.

Amemtaka Mbunge huyo (Kigua) ambaye ni Mwanachama wa NBAA awe anaingia kwenye akaunti yake na kupandisha ratiba ya kikao husika na uthibitisho wa mahudhurio katika mkutano husika ili masaa yake yahesabiwe.

Wabunge wengine waliochangia kwenye hoja hiyo wakitaka taaluma zitambuliwe na kulipiwa gharama za ushiriki wa mikutano ni Issa Mtemvu aliyehoji kwa wanasheria huku Waziri Dk Mwigulu Nchemba naye alieleza kama itapitishwa basi na wachumi watambuliwe.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Ester Matiko yeye alipendekeza Bunge liwatambue wabunge waliohudumu muda mrefu kwenye kamati za LAAC, PAC na Kamati ya Bajeti watambue na kupewa CPA za heshima.

Dk Mwigulu amesema jambo hilo siyo geni kwani liliwahi kutokea kwa Marehmu Elias Kwandikwa ambaye alipewa Uhandisi wa heshima kutokana na mchango wake kwenye Wizara ya Ujenzi.