Mtwara. Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hassan Mtenga amekitaka chama hicho kuwachukulia hatua kali wale aliowataja kuwa ‘wahuni’ waliomo ndani ya chama hicho wanaovujisha taarifa kwa wapinzani na kupanga mikakati ya kuhujumu mafanikio ya Serikali.
Mtenga ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 14, 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Chikongola, Mtwara.
Kwa mujibu wa Mtenga, akiwa mbunge aliyewakilisha Mtwara Mjini kwa miaka mitano, amesema kuna watu aliowaita ‘wahuni’ ambao wanakwenda kuwatia sumu wananchi ili waishukie CCM na watu hao wamo ndani ya chama hicho.

“Ukweli lazima usemwe, kuna wahuni hapa Mtwara ambao wanakwenda kuwatia sumu wananchi na hawa wahuni wako ndani ya CCM, hili halikubaliki. Anakuja mtu mmoja anampa Heche (John Heche-Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara) karatasi yenye maelezo kuhusu hali ya korosho. Huyu si mtu wa kumchekea. Wahindi wote walikuja, yeye alikuwa anapanga bei ya korosho.
“Nashukuru Rais na Waziri Bashe Hussen Bashe (Waziri wa Kilimo) kwa kuwatengua, sasa wako chali, lakini chama kimshughulikie mtu huyu vikali, kwani anatengeneza chuki,” amesema Mtenga bila kumtaja mtu huyo.
Alichosema Heche
Katika ziara yake mkoani Mtwara siku chache zilizopita, Heche alisema kumekuwa na makato makubwa kwa wakulima wa korosho huku akienda mbali zaidi kwa kusema hata lugha inayotumika imekuwa siyo rafiki kwa wakulima hao, kwani ni Kiingereza.
“Nataka kushughulika na hawa watu kwa namna wanavyonyonya wananchi, haya hapa ni makato yanayofanywa katika kila kilo moja ya korosho, ambapo mkulima anakatwa asilimia 25 kwenye kila kilo moja, na wanaandika kwa Kiingereza ili msiweze kuelewa.
“Wakati mwingine nikisema Sh25 wewe unaweza usielewe, lakini kiwango hicho kinapelekwa bodi ya korosho kwa hiyo fedha yako inatumika kwenda kuendesha bodi ya korosho ilihali wewe ndiye unahangaika na kilimo cha korosho na familia yako ila siku tu ukivuna wanakuja. Vyama vya ushirika wanachukua Sh120 kwenye kila kilo, lakini wanakwambieni nyie hizi anakatwa mnunuzi,” alisema Heche huku akiwa na orodha ya tozo hizo.
Maelezo ya Makalla
Makalla kwa upande wake, amesema mafanikio mengi yaliyopatikana chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni ya kihistoria, hasa kwenye sekta ya kilimo, barabara, bandari na elimu na kwamba wapinzani wanajisumbua.

“Safari ya mafanikio ya wakulima wa korosho imeanza muda mrefu. Sasa foleni za magari kusafirisha korosho kwenda Dar hazipo tena, bandari ya Mtwara imeboreshwa. Rais ameshusha Sh800 bilioni kwa ujenzi wa barabara,” amesema Makalla.
Makalla pia amesisitiza uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 upo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba maandalizi yamekamilika ndani ya CCM.
“Tutashiriki uchaguzi tukiwa tumejiandaa,” amesema.
Aidha, Makalla amewataka Watanzania kupuuza wanasiasa wanaohubiri uvunjifu wa amani.
“Hatutakubali mtu achezee amani yetu. Tutashindana kwa hoja na kwa kutumia kampeni za kistaarabu zitakazoongozwa na falsafa ya 4R za Rais Samia,” amesema.
Katika mkutano huo, wazee wa kimila wa kabila la Wamakonde wamempa Makalla uchifu na jina la heshima la “Mpakua” na kumkabidhi vazi na kofia kama ishara ya utulivu na imani yao kwake.
Mapema, aliyekuwa Katibu wa Chadema, Wilaya ya Lindi Mjini, Hamis Mtanda, alitangaza kujivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na CCM.
Mtanda ametambulishwa rasmi leo na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Mtama.
“Walisema operesheni zao watazipigia kambi Mtama, mimi nimeenda kupiga kwenye mshono. Ninamleta kwenu katibu wa Chadema wa wilaya, ngoma ya watoto haikeshi, na mimi ndiye simba wa kusini. Kiburi chao kilikuwa huyu jamaa, amemwaga manyanga amerudi kwenye gari,” amesema Nape.

Makalla yuko katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM mikoa ya Lindi na Mtwara.
Makalla anatarajiwa kuendelea na ziara yake kuelekea wilayani Nanyamba kwa ajili ya kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ya mwaka 2020-2025.