Mbunge aibana Serikali, idara ya uhamiaji kujenga zahanati Z’bar

Dodoma. Mbunge wa Dimani, Mustafa Mwinyikondo Rajab ameihoji idara ya uhamiaji ina mpango gani wa kujenga hospitali Zanzibar kama ilivyo kwa vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Mbunge huyo amesema vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamejenga zahanati na hospitali ambazo zinasaidia kutoa huduma ambazo hata wananchi wananufaika nazo, lakini uhamiaji hawajafanya hivyo.

Akijibu swali hilo bungeni leo Jumatano Mei 7, 2025 jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema Serikali kupitia idara hiyo inafanya maandalizi ya kujenga zahanati katika maeneo hayo.

”Kama ilivyo kwa vyombo vingine vya ulinzi na usalama idara ya uhamiaji ina mpango wa kuwa na zahanati kwa lengo la kutoa huduma za afya kwa watumishi na jamii inayoizunguka,” amesema Sillo.

Amesema Serikali kupitia idara ya uhamiaji imefanya mawasiliano ya awali na Wizara ya Afya ya Zanzibar,  ili kupata mwongozo kuhusu namna bora ya uanzishwaji wa zahanati itakayokidhi mahitaji kwa jamii itakayohudumiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *