
Wanafunzi wengi wamekuwa wakipata wakati mgumu na tabu katika kuhifadhi yale wanayofundishwa, ama kwa sababu ya tofauti ya uwezo wao wa akili au kwa sababu ya uvivu.
Leo nataka tuzitazame njia tano ambazo mwananafunzi yeyote anaweza kuzitumia kuhifadhi yale aliyofundishwa kwa njia rahisi zaidi.
Mosi, kurudia rudia yale aliyofunzwa. Hii ndiyo njia mama ya kuhifadhi chochote hata kama ni kigumu vipi. Kitu chochote kikirudiwa mara nyingi zaidi, hugeuka kutoka katika hali ya ugumu na kuwa chepesi.
Pili, kuhusianisha vitu. Kwa mfano, kama mwanafunzi anafundishwa mada ya idadi ya watu (population) kinachotakiwa kuja akilini haraka sana ni maeneo yote yenye asili ya watu wengi kama Kariakoo, Mbagala na kwengineko.Hii itamsadia kukumbuka kwa haraka sana.
Tatu, kuwaelekeza wanafunzi wengine. Mwanafunzi anapokuwa anawaelekeza wenzake katika somo fulani au mada fulani, kitendo hicho kinamsaidia kuhifadhi, kukumbuka na kuelewa zaidi na zaidi.
Baadhi ya wanafunzi wana mtazamo hasi kuwa kuwafunza wengine kunaondoa waliyohifadhi, mtazamo ambao siyo kweli hata kidogo.
Nne, njia ya kutengeneza vifupisho (mnemonics). Hii ni njia nzuri na nyepesi sana ambayo inamsaidia mwanafunzi kuhifadhi taarifa nyingi akilini bila kusahau tena kwa mpangalio.
Kwa mfano, tuchukulie mwanafunzi amefundishwa vitu vitano ambavyo vilikuwa ni vivutio vikubwa vya wakoloni kama vile; maeneo kwa ajili ya uwekezaji (areas for investment), watumwa (cheap labour),maeneo kwa ajili ya makazi (areas for settlement), malighafi (raw materials) na soko (market).
Kanuni yake inaweza kuwa (AREAREMACHERA-Tamka kama ilivyoandikwa); Are(Area for Investment); Are(Area for settlement); Ma(Market); Che(Cheap labors); Ra(Raw materials).
Tano, kusoma kwa kuongea mwenyewe kwa sauti ya chini ambayo inamtosheleza msomaji mwenyewe.
Njia hii ina faida nyingi,ikiwemo kuhifadhi kwa urahisi na mbili ni kuuzoesha ulimi matamshi ya lugha ambayo mwanafunzi anaitumia.
Mara nyingi hii huwa ni changamoto kwa wanafunzi walio wengi ,kwani wanakuwa na uwezo mkubwa wa kuandika lakini siyo kuzungumza lugha. Hii ni kutokana na changamoto ya mfumo wa usomaji wa kusoma kimya kimya tu bila kuongea.
0714172736/ shasanyaseminars@gmail