Dar es Salaam. Hivi karibuni kulikuwa na tetesi nyingi za timu kubwa Afrika kuwahitaji wachezaji wa Yanga ambao wamekuwa kwenye viwango bora baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika lakini uongozi wa timu hiyo iligomea hilo pamoja na kudaiwa kutajiwa kitita kikubwa cha fedha.
Msimu wa mwaka 2022/2023, Yanga ilifanikiwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria ambapo haikufanikiwa kutwaa ubingwa kwa kanuni ya bao la ugenini waliyopata USM Alger kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Dar es Salaam ambapo Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1.
Kwenye mechi ya marudiano Yanga ilishinda bao 1-0 uko nchini Algeria, hivyo kuzidiwa idadi ya mabao na USM Alger ikatwaa ubingwa huo.
Msimu uliofuata wa mwaka 2023/2024, Yanga ilicheza mashindano ya Klabu Bingwa Afrika lakini pasipo kuwa na mshambuliaji wao hatari wa msimu wa 2022/23, Fiston Mayele ambaye alitimkia kwenye Klabu ya Pyramids ya Misri na pengo lake lilionekana moja kwa moja.

Kitendo cha Mayele kuondoka Yanga kiliwapa wakati mgumu viongozi na benchi la ufundi kuingia sokoni kusaka mshambuliaji mpya.
Haikuwa rahisi kupata mchezaji mwingine kama Mayele ikabidi kocha iwatumie washambuliaji waliokuwepo Kennedy Musonda na Clement Mzize kabla ya kumleta Joseph Guede ambaye naye hakuonyesha makali waliyotarajia akaondoka.
Yanga ilicheza Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwategemea zaidi Musonda na Mzize kama washambuliaji vinara huku Joseph Guede akionekana siyo chaguo la kwanza kwa kocha Miguel Gamondi.
Kwenye hatua ya makundi, Yanga ilifanya vizuri baada ya kumaliza nafasi ya pili ambapo ilikusanya pointi nane nyuma ya Al Ahly ambao walikuwa vinara wa kundi wakiwa na pointi 12, wakati CR Belouzdad na Madeama zilishika nafasi ya tatu na nne.
Kwenye hatua ya robo fainali, Yanga iliondolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika kwa mikwaju ya penalti.
Pointi ya msingi
Imekuwa ni kawaida kwa timu kubwa hapa Afrika kuchukua wachezaji walioonyesha viwango bora msimu uliomalizika kwenye timu za kawaida ambazo haziwezi kushindana kiuchumi.
Mfano baada ya Simba kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ilifanya biashara ya wachezaji mahiri wa timu hiyo wakichukuliwa na timu kubwa ambapo Luis Miquissone alitimkia Misri kwenye Klabu ya Al Ahly huku Clatous Chama akienda RS Berkane ya Morocco, ambako walinunuliwa kwa pesa nyingi ili timu hizo ziweze kujidhatiti na kuwania makombe, kweli Ahly ilitwaa Ligi ya Mabingwa.
Kuondoka wachezaji muhimu, msimu uliofuata Simba ilijikuta kwenye wakati mgumu wa kutafuta mbadala wa wachezaji wengine watakaofanya vizuri kikosini, lakini mambo yakawa magumu.
Kadri walivyozidi kutengeneza kikosi kuwa kama kile cha misimu ya nyuma ndivyo walivyozidi kupitia nyakati ngumu kwenye mashindano mbalimbali ambapo msimu uliofuata ilishindwa hata kufuzu hatua ya makundi baada ya kuondolewa na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ukiachilia mbali kufanya vibaya kwenye mashindano ya kimataifa, Simba ilijikuta ikifanya vibaya hata kwenye mashindano ya ndani ambapo ilipoteza taji la Ligi Kuu na watani wao wa jadi Yanga msimu wa 2021/2022, pamoja na Kombe la FA ambapo iliambulia Kombe la Mapinduzi tu.
Ni misimu mitatu imepita tangu Simba ilipochukua ubingwa msimu wa mwaka 2020/2021, ambapo ilitwaa ubingwa mara nne mfululizo kabla ya Yanga kuvunja utawala ambao mpaka sasa ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu wakiwa wamebeba mara tatu.
Chanzo cha kufanya vibaya
Kuondoka kwa wachezaji muhimu wa kikosi cha Simba kama Clatous Chama na Luis Miquissone wakati huo kitendo hicho kilisababisha kikosi cha wekundu wa Msimbazi kukosa muunganiko mzuri kama ule uliyokuwepo kipindi cha nyuma.
Uongozi wa Simba pamoja na kwamba ulikuwa na fedha lakini ulishindwa kutafuta wachezaji wazuri ambao wangeweza kuziba nafasi za wachezaji walioondoka ili kuendelea kuwa na kikosi bora ni sababu nyingine ambayo imewafikisha hapa walipo.
Usajili mzuri wa wachezaji uliyofanywa na rais wa Yanga Hersi Said, umeifanya Yanga kutamba misimu mitatu ikifanya vizuri kwa kutwaa mataji mbalimbali ambapo mpaka sasa imeshachukua jumla ya mataji 10 ndani ya miaka mitatu pekee lakini pia imefanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa, hivyo ni jambo moja tu Yanga inatakiwa kufanya kuwalinda mastaa wake wasiondoke ili iweze kutwaa mataji Afrika au kuwaachia waende wakawasaidie wapinzani wao kutwaa mataji yaleyale ambayo inawania.
Je, suluhisho la haya ni nini?
“Klabu ikiwa inataka kufanya vizuri kwenye mashindano haiwezi ikamuachia mchezaji bora aondoke kwa kuwa ni jambo gumu kumpata mwingine,” alisema hayo Ally Kamwe Ofisa habari wa Yanga alipokuwa akiwajibu waandishi wa habari kuhusu tetesi zilizokuwa zinamhusu mshambuliaji wao Clement Mzize kutakiwa na Klabu ya Wydad Athletic ya Morocco.

Kuwabakiza mastaa
Licha ya wachezaji nyota wa Yanga kama Stephane Aziz Ki, Clement Mzize, Max Nzengeli na Pacome Zouzoua kumezewa mate na timu kubwa Afrika pamoja na nyingine kudaiwa kupeleka ofa lakini Yanga ilifanikiwa kuwaongezea mikataba nyota wake mbele ya vigogo wa Afrika jambo ambalo si kawaida kwa timu zenye uchumi wa kati kufanya hivyo.

Timu nyingine zinapaswa kujifunza kutoka kwa Yanga imeonekana ndiyo njia pekee ya kulinda ubora wa timu usipotee kwani kuondoka kwa wachezaji bora kunarudisha nyuma uimara wa timu na kuwafaidisha wapinzani ambao timu hizo zimekuwa zikiwania nao ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Unaweza kufikiria ni kwanini Klabu ya Al Ahly inaendelea kufanya vizuri kila msimu na haiuzi nyota zake zaidi ya kununua wapya, jibu lake ni kwamba Al Ahly haiwezi kuacha wachezaji bora waondoke na ndiyo maana inatumia fedha nyingi kutafuta wachezaji kuliko kupata fedha nyingi kutokana na kuwauza.
Iwapo Yanga ikiendelea kuwabakiza wachezaji bora kwenye timu na kufanya usajili wa wengine wachache ndani ya misimu michache itafikia mafanikio ya wakubwa wa bara la Afrika ya kutwaa mataji.