
LONDON, ENGLAND. Baada ya msimu uliopita kumaliza nafasi ya sita ikiambulia kufuzu michuano ya Uefa Conference League, Chelsea imeonekana kung’aa na kuanza vizuri zaidi msimu huu ikishinda mechi tano, sare mbili na kupoteza mbili kwenye mechi tisa za Ligi Kuu England ikiwa inashika nafasi ya tano.
Katika msimu uliopita hadi kufikia mechi ya tisa ilishapoteza mechi tatu, ikashinda tatu na kutoa sare tatu ikiwa na pointi 12 wakati msimu huu katika mechi hizo imekusanya pointi 17.
Mbali ya matokeo kikosi cha Chelsea kimeonekana kubadilika zaidi chini ya kocha huyu kuanzia uchezaji wa timu kiujumla na viwango vya mchezaji mmoja kwa mmoja.
Hata hivyo, mbali ya mambo ya ndani ya uwanja ikiwa pamoja na mbinu, taarifa zinaeleza kocha wa matajiri hawa wa Jiji la London, Enzo Maresca amebadilisha mambo mengi yanayofanya wachezaji wawe na hali ya kupambana na timu kupata matokeo.
Kwa mujibu wa The Sun, moja kati ya changamoto alizokutana nazo ilikuwa ni wachezaji kutokuwa na furaha juu ya kile kilichokuwa kinaendelea kwenye timu hiyo.
Kwanza kulikuwa na mastaa wengi kiasi cha kupokezana wakati wa kufanya mazoezi ambapo kulikuwa na makundi mawili na muda mwingine matatu.
Baadhi ya wachezaji pia walilazimika kwenda kwenye timu za vijana kwa ajili ya mazoezi kwa sababu ya wingi wao.
Pia wakati anatua kulikuwa na suala la Enzo Fernandes ambaye video yake ilisambaa akiwa anaimba nyimbo ambayo ilitafsiriwa kuwa ni ya kibaguzi kwa wachezaji wanaotokea Ufaransa.
Maresca alifanikiwa kuwatuliza wachezaji wake raia wa Ufaransa ambao walikuwa wamechukizwa na tukio hilo na kila kitu kikawa.
Wachezaji wameripotiwa kuwa na furaha sana chini yake kwa sababu ya mbinu anazotumia kuwafanya wawe pamoja na wenye furaha.
Kwanza mazoezini amekuwa akiwapa uhuru wa kuchezea mpira zaidi tofauti na ilivyokuwa kwa makocha waliopita ambao walihitaji mastaa wafanye zaidi mazoezi ya kimwili.
Mbali ya kuwafanya wachezee sana mpira, pia Maresca muda mwingine huwa anakuwa mmoja kati ya wachezaji na hufanya nao mazoezi.
Kocha huyu wa zamani wa Manchester City na West Ham pia ameanzisha utaratibu wa kuwashangilia ama kuwapongeza wachezaji waliopata mafanikio ya aina flani ambao huwa wanapewa gwaride la heshima.
Vilevile wanapokuwa katika mazoezi ya Gym, huwa wanashindanishwa wachezaji kwa wachezaji hali ambayo husaidia pia kuongeza utimamu wao wa kimwili.
Chelsea ambayo juzi ilishindwa kutinga hatua ya robo fainali ya Carabao Cup baada ya kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Newcastle ni miongoni mwa timu ambazo hazijapoteza hata mechi moja katika michuano ya Conference League ambapo katika mechi mbili imeshinda mbili.