
Bila shaka tumeshakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mtaji na namna ya kuulinda. Lakini jambo lingine muhimu ni namna ya kukuza mtaji wa biashara. Ukuzaji wa mtaji ni muhimu kwa sababu mtaji ndio msingi wa ukuaji na maendeleo ya biashara yoyote, hasa kwa wafanyabiashara wadogo.
Mtaji wa kutosha unamudu mfanyabiashara kununua bidhaa za ziada au kuboresha vifaa vya kazi, hivyo kuongeza uzalishaji na mauzo. Mtaji pia hukinga biashara dhidi ya changamoto zisizotarajiwa kama gharama za ghafla au kupungua kwa soko, hivyo kuhakikisha uendelevu.
Ni vizuri kukuza mtaji wa biashara, kwani unasaidia mfanyabiashara kupata uhuru wa kifedha, kupunguza utegemezi wa mikopo ya riba kubwa ambayo inaweza kuingiza biashara kwenye madeni yasiyolipika. Mtaji ni nguvu ya kuendesha biashara mbele na kuhakikisha inastawi katika mazingira yenye ushindani.
Kwa mfanyabiashara mdogo, kukuza mtaji ni jambo linalowezekana kwa kutumia mbinu za vitendo zinazolingana na rasilimali zilizopo. Hizi hapa mbinu za msingi za kuzingatia:
1. Kuongeza mauzo kwa uuzaji wa ndani: Bila kuwa na soko la uhakika wa biashara yako ni ngumu kuweza kukuza mtaji wako. Ni vema kutenga fedha na muda wa kutangaza bidhaa ama huduma unayoiuza kwa wateja wako.
Tangaza kwa gharama nafuu kwa kutumia njia ambazo unaweza kuzimudu kama vile vipeperushi, mitandao ya kijamii, kuweka mabango kwenye masoko, au kutumia redio za jamii. Kwa mfano, akiuza nguo, anaweza kutoa ofa kwa wateja wa mara kwa mara ili kuwavutia wengine. Mauzo ya ziada yanamaanisha faida zaidi ya kuwekeza tena.
2. Kupunguza matumizi ya ziada: Nunua kwa jumla ili uweze kupata punguzo. Ni vizuri kama unafanya biashara ya kuuza na kununua kwa jumla ama kiwandani moja kwa moja. Kufanya hivyo kunaweza pia kupunguza gharama za usafiri.
Unaweza pia kuunganisha safari za ununuzi au kutumia wafanyakazi wachache lakini wenye ujuzi wa kutosha. Hii inaokoa pesa kwa ajili ya biashara na kukuwezesha kupata faida na hivyo kukuza mtaji wako.
3. Kutafuta mikopo midogomidogo: Taasisi ndogo za kifedha au vikundi vya akiba (kama Vicoba na Saccos) hutoa mikopo ya haraka na ya riba nafuu kwa wafanyabiashara wadogo. Kabla ya kukopa, ni muhimu kuwa na mpango wa jinsi fedha za mkopo zitakavyotumika, kama kununua mashine au kuongeza malighafi ili kuhakikisha faida inayolipa mkopo na ziada ili kukuza mtaji.
4. Kuweka akiba na kuwekeza: Kama ambavyo mtu binafsi anaweza kuweka akiba, ni vema pia biashara ikawa na akiba yake kwa ajili ya matumizi ya baadaye ya kuongeza bidhaa au tawi jingine la biashara.
5. Kushirikiana na wengine: Biashara ni ushirikiano wa namna tofauti. Ni nadra kufanikiwa kama unakuwa huna ushirikiano au ushiriki na wengine, huwajali wateja ama wafanyabiashara wengine.
Ni vema kuingia kwenye vyama vya wafanyabiashara, kuwa na kikundi cha kuweka akiba na wafanyabiashara wengine. Mnaweza kubadilishana mawazo, kupata elimu na maarifa yanayoweza kupeleka biashara yako kwenye malengo uliyojipangia.
Kwa kutumia mbinu hizi, mfanyabiashara mdogo anaweza kukuza mtaji wake hatua kwa hatua bila kujihusisha na hatari kubwa, akijenga Biashara thabiti na yenye tija kwa muda mrefu.