Mbeya yaanza mchakato kuligawa jimbo la Dk Tulia

Mbeya. Halmashauri ya Jiji la Mbeya imependekeza kuanza mchakato wa kuchunguza na kuligawa Jimbo la Mbeya Mjini kupata jimbo jipya la Uyole, katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, 2025.

Mchakato huo ukikamilika na kukidhi vigezo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) italitangaza jimbo jipya, jambo ambalo litakuwa jawabu la matakwa ya wakazi wa Mbeya Mjini.

Mei 3, 2023, bungeni Dodoma, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Hamisi Nderiananga alidokeza kuwa, Dk Ackson ni miongoni wa wabunge waliowasilisha maombi ya kugawa majimbo yao kuwa mawili kutokana na ukubwa na wingi wa watu.

Nderiananga alikuwa akijibu swali la nyongeza la Sophia Mwakagenda, mbunge wa Viti Maalumu aliyeuliza ni lini Serikali italigawa jimbo la Mbeya Mjini kutokana na ukubwa wake.

Akizungumza niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa jiji hilo, John Nchimbi leo Machi 11, 2025 katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala jijini humo, Nicodemus Tindwa amesema hatua hiyo ni baada ya kupokea barua kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Amesema Jimbo la Mbeya Mjini lina tarafa mbili, kata 36, mitaa 181 na eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 258.8 na kwamba baada ya majadiliano na uchambuzi wa kina wa menejimenti ya halmashauri hiyo, walikubaliana jimbo hilo ligawanywe kupata jimbo jipya la Uyole.

“Kugawanywa kwa jimbo hili ni kupanua wigo wa uwakilishi wa wananchi na kufikisha huduma ya uwakilishi kwa njia bora kwa ufanisi na haraka, lakini tumechambua vigezo kuwa Jimbo la Mbeya Mjini liwe na wakazi 600,000 na Uyole 400,000.

“Kwa sasa Jimbo la Mbeya Mjini linakadiriwa kuwa na watu 682,264 bila kujumuisha wale wanaoingia na kutoka mchana na usiku kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii,” amesema Nicodemus.

Nicodemus ameongeza kuwa kwa kuzingatia uwiano wa watu, Jimbo la Mbeya Mjini litakuwa na idadi ya watu 254,746 na kata 23, huku jimbo la Uyole likiwa na kata 13 na watu 286,857.

“Jimbo la Mbeya Mjini litakuwa na kata za Forest, Ghana, Iganzo, Isanga, Itagano, Itende, Itiji, Iwambi, Iyela, Iyunga, Iziwa, Kalobe, Maanga, Mabatini, Maendeleo, Majengo, Mbalizi Road, Nonde, Nsoho, Nzovwe, Ruanda, Sinde na Sisimba.

“Uyole itakuwa na kata za Mwansenkwa, Ilemi, Ilomba, Mwakibete Iduda, Iganjo, Igawilo, Isyesye, Itezi, Mwasanga, Nsalaga, Tembela na Uyole,” amesema mtumishi huyo mwandamizi.

Akizungumzia hatua hiyo, Diwani wa Kata ya Nsalaga, Daud Ngogo amesema mapendekezo hayo ni kilio chao cha muda mrefu, akieleza kuwa kuwapo kwa jimbo hilo kunaenda kufungua fursa mpya za kiuchumi na maendeleo kwa wananchi.

“Ina maana hata halmashauri tutapata, huduma zitawafikia wananchi kwa urahisi na kufungua fursa zaidi kiuchumi. Tangu 2023 tulikuwa tukipambana kupata majimbo mawili, hivyo sasa ni wakati mwafaka,” amesema Ngogo.

Kwa upande wake, Diwani Viti Maalumu, Agatha Ngole amesema huduma za kijamii ikiwamo barabara, vituo vya afya na zahanati pamoja maji, pia kupanua fursa nyingine za kiuchumi kwa wananchi zitaongezeka.

Baadhi ya madiwani wa Jiji la Mbeya wakiwa katika kikao maalumu ambacho kimependekeza na kukubaliana Jimbo la Mbeya Mjini kugawanywa kupata Jimbo jipya la Uyole.

“Tunapongeza kwa kuwa tulisubiri sana mgawanyo, tunaenda kupata wawakilishi wawili bungeni, hivyo kufanya huduma za wananchi kupatikana kirahisi, madiwani tunaomba hili lifanyike,” amesema Agatha.

Mchambuzi wa siasa jijini Mbeya, Chifu Mwaihojo Mwambipile amesema pamoja na kugawanywa kwa majimbo, wananchi wajiandae kuchagua kiongozi mwenye maono badala ya kuchagua chama.

“Waachane na viongozi wanaoangalia makundi ya upande fulani kama bodaboda au bajaji, waangalie mtu mwenye maono kusaidia maendeleo, Serikali inaweza kufanya kazi na mtu yeyote aliye tayari kuleta mabadiliko,” amesema Mwambipile.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *