Mbeya izipiganie KenGold, Tanzania Prisons

Msimamo wa ligi hiyo ulivyo, unaonyesha wazi namna ligi hiyo ilivyogawanyika makundi matatu hivi sasa kutegemeana na nafasi ambazo timu zipo kwenye msimamo wa ligi na idadi ya pointi ambazo kila moja imekusanya.

Kundi la kwanza ni la timu ambazo zinapigania ubingwa ambalo lenyewe linahusisha timu tatu ambazo ni Yanga inayoongoza msimamo wa ligi, Simba iliyo nafasi ya pili na Azam FC inayoshika nafasi ya tatu.

Kuna kundi la timu ambazo kimahesabu zimeshajihakikishia kubaki Ligi Kuu ambazo ni Simba, Yanga, Azam, Singida Black Stars na  Tabora  United ingawa pia kuna JKT Tanzania ambayo kuna uwezekano finyu wa kushuka japo ina pointi 30.

Halafu kuna timu ambazo zipo katika hali ngumu na hivi sasa kila moja ina mechi saba za kujitetea ili iweze kubakia Ligi Kuu vinginevyo zitakazoshindwa kufanya vizuri zitapewa mkono wa kwa heri na kuangukia katika Ligi ya Championship.

Timu hizo 10 ambazo hadi sasa haziko salama ni Fountain Gate, Dodoma Jiji, Coastal Union, KMC, Mashujaa, Namungo, Pamba, Kagera Sugar, Tanzania Prisons na KenGold.

Presha inaonekana kuwa kubwa zaidi kwa Tanzania Prisons ambayo ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 18 na KenGold iliyopo katika nafasi ya mwisho ikiwa na pointi 16.

Mwenendo ambao Tanzania Prisons imekuwa nao katika siku za hivi karibuni umekuwa sio mzuri kwani wachezaji wake wamekuwa hawachezi vyema ndani ya uwanja na wamekuwa wakifanya makosa ya mara kwa mara yanayopelekea timu hiyo ifanye vibaya.

Hilo linaweza kujidhihirisha kwa mechi 10 zilizopita za Ligi ambapo Maafande hao wamepata ushindi mara mbili na kutoka sare moja na wamepoteza michezo saba.

Na ushindi katika mechi hizo mbili ulipatikana kwa mechi moja iliyochezwa mechi iliyochezwa mwishoni mwa mwaka jana na ya mwisho ikawa mwezi Februari mwaka huu na baada ya hapo ikacheza mechi sita mfululizo bila kupata ushindi.

KenGold baada ya kufanya vibaya katika mechi nyingi za mzunguko wa kwanza, baada ya kipindi cha usajili wa dirisha dogo lililofungwa Januari 15 mwaka huu, ilionesha ishara ya kuimarika kwa kupata ushindi mara mbili katika mechi nne zilizochezwa ikafikisha pointi 13 ambazo zilianza kuonyesha mwanga kwao kwamba wanaweza kuondoka katika presha ya kukaa mkiani.

Kwa timu kama KenGold na magumu iliyopitia mwanzo, ilipaswa kuhakikisha inakuwa na muendelezo wa kufanya vizuri angalau kupata pointi sita au saba kwenye mechi tatu ambazo ilicheza baada ya hapo dhidi ya JKT Tanzania, KMC na Mashujaa.

Bahati nzuri kwao michezo dhidi ya KMC na Mashujaa ilikuwa katika Uwanja wake wa nyumbani wa Sokoine Mbeya lakini ilijikuta ikitoka sare yote kama ambavyo ilifanya ugenini dhidi ya JKT Tanzania.

Kama ingefanikiwa kupata ushindi katika mechi angalau mbili kati ya hizo, leo hii tungekuwa tunaizungumzia KenGold kama timu ambayo haipo katika nafasi mbili za mwisho kwenye msimamo wa ligi ambazo mwishoni mwa msimu zitashuka daraja moja kwa moja.

Kitendo cha timu mbili za mkoa wa Mbeya kuwa katika uwezekano mkubwa wa kushuka daraja kwa pamoja, sio jambo ambalo wakazi wa mkoa huo wanapaswa kuliruhusu litokee kwa msimu huu kwani kitaacha pigo kubwa kwa  mkoa husika na sio klabu hizo pekee.

Zikishuka Maana yake kuna fungu kubwa la mapato ambayo yatakosekana kwa mkoa  lakini pia wengi watapoteza kipato cha mtu mmoja mmoja ambacho hupatikana pindi kunapochezwa mechi za ligi mkoani humo.

Zipo athari nyingi ambazo Mbeya inaweza kukutana nazo iwapo haitakuwa na timu kwenye Ligi Kuu ambayo ndio daraja la juu zaidi la ligi hapa nchini kama hizo baadhi nilizotaja hapo juu.

Mbeya haipaswi kuona anguko la Tanzania Prisons na KenGold kama litakuwa la klabu hizo  pekee bali pia ilione kama jinamizi litakalokuja kuutesa mkoa mzima siku za usoni.

Kufanya vizuri kwa Mbeya City katika Ligi ya Championship hakupaswi kuufanya mkoa wa Mbeya usione haja ya kuzipambania KenGold na Tanzania Prisons kwani inawezekana pia Mbeya City ikashindwa kupanda Ligi Kuu na ikaishia kuacha maumivu mara mbili kwa mashabiki wa soka mkoani humo.

Mechi saba ambazo timu hizo kila moja imebakiza zinaweza kuleta ukombozi kwao ikiwa mkoa mzima utaziunga mkono kwa mechi zote ambazo zitacheza kwenye Uwanja wa Sokoine na zile ambazo zitachezwa ugenini.

Jukumu la kuziokoa timu hizo halipaswi kuwa la watu wachache bali wengi wenye mapenzi mema na Mpira wa miguu mkoa wa Mbeya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *