Mbaroni kwa kukutwa na nyama, ngozi na vichwa vitatu vya swala

Liwale. Jeshi la Polisi mkoani Lindi kwa kushirikiana na askari wa hifadhi ya wanyamapori wamemkamata mkazi wa Kijiji cha Chimbuko, Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi, Ramji Kassim Kijambiko (36), akituhumiwa kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Kijambiko ambaye ni  mtuhumiwa alikamatwa mnamo  Februari 25,2025, saa 11:00, akiwa na vipande 21 vya nyama mbichi ya swala, vichwa vitatu vya swala, ngozi tatu za swala, pamoja na nyaya tatu zinazotumika kama mitego ya kuwakamata wanyamapori.

Nyara hizo zinakadiriwa kuwa  na thamani ya  Sh3.03 milioni imefafanua taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtuhumiwa alikuwa akitumia mbinu ya kuweka mitego ya nyaya ili kuwakamata swala, kisha kuwachinja na kuwauza kinyume cha sheria.

Kitendo hicho ni uvunjifu wa sheria za uhifadhi wa wanyamapori, ambazo zinakataza uwindaji haramu na biashara ya nyara za Serikali bila kibali.

Jeshi hilo  limewataka  wananchi kufuata taratibu za kisheria katika uwindaji ili kulinda wanyamapori na mazingira kwa ujumla.

Pia wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kuhusu vitendo vyovyote vya uwindaji haramu.