
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma za chakula na vinywaji, ikiwa ni sehemu ya kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia mradi wa reli ya kisasa (SGR).
Katika kutekeleza hilo, amesisitiza ni muhimu shirika hilo kuhakikisha linashirikiana na sekta binafsi katika kusaidia maendeleo ya miundombinu ya taifa.
Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo Jumanne, Februari 11, 2025 wakati wa ufunguzi wa mgahawa wa 11 wa KFC unaomilikiwa na Kampuni ya Dough Works Limited (DWL), katika stesheni ya SGR Magufuli jijini Dar es Salaam.
Amesema mgahawa huo mpya utaongeza urahisi kwa wasafiri kupata huduma mbalimbali, kama vile za chakula na vinywaji, kutengeneza nafasi za ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.
Akitoa maelekezo, Profesa Mbarawa amesema Serikali bado inaamini kuna fursa nyingi kupitia mradi huo, hivyo ameiagiza TRC kuhakikisha inatoa mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji.
“DWL alipokuja kwangu sikuchukua muda mrefu kufanya maamuzi, TRC pia mlifanya jambo sahihi kwa muda sahihi na leo matokeo chanya yanaonekana. Pili bado tunaamini ipo fursa ya migahawa katika SGR yetu, nendeni mkakae na wafanyabiashara husika.”
Ametaja eneo la tatu analotaka lifanyiwe kazi kuwa ni maduka ya vitu vidogo vidogo.
“Wasafiri hukumbuka mahitaji yao dakika za mwisho, kwa mfano dawa muhimu. Kuwa na duka la dawa za binadamu, hii italeta fursa kwetu kama TRC na pia italeta hamasa kwa wasafiri wetu.”
“Pia tafuteni watakaoleta maduka ya zawadi, kuna watu wageni kutoka Dodoma, Mwanza na nje ya nchi wanaokwenda Dodoma au Morogoro na vituo vya njiani kutembelea ndugu na jamaa,” amesema.
Mbarawa amesema anataka kuona huduma za kifedha zinakuwa nyingi, watoa huduma wa benki zote na huduma za kifedha kupitia mitandao yote ya simu zikipatikana zitachangia kutoa huduma zinazoendana na wakati kwa wateja.
“Tunataka tuone maduka ya huduma za teknolojia. Pia nawalekeza KFC mhakikishe huduma hii inakuwa endelevu kwa kuweka vituo vingine Morogoro na Dodoma. Wasafiri ndiyo hao hao wanaotoka Dodoma kuja Dar es Salaam, lazima muweke kituo cha pili Dodoma na kituo cha tatu kiwe Morogoro,” amesema Mbarawa.
Mkurugenzi Mkuu wa DWL, Vikram Desai amesema mgahawa huo unatazamiwa kuhudumia wafanyakazi wa SGR, wasafiri wa kila siku na wa masafa marefu.
Amesema mgahawa huo unasaidia moja kwa moja ajenda ya uchumi wa Tanzania kwa kutengeneza ajira mpya kwa vijana, kutoa mafunzo na ukuaji wa taaluma ndani ya tasnia ya huduma ya chakula.
“Tumejitolea kukuza uchumi kwa kutengeneza ajira na kutoa uzoefu wetu wa kutengeneza chakula chenye viwango. Uanzishwaji huu unaleta ubora na urahisi kwa Watanzania wengi huku tukisaidia wauzaji bidhaa, wafugaji na wafanyabiashara wa ndani,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirikala Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema “uzinduzi wa mgahawa huo ni muhimu kwa abiria na kuhamasisha uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya reli.”