Mbappe, Rudiger wapigwa rungu, kuivaa Arsenal

Nyota wa Real Madrid Antonio Rudiger, Kylian Mbappe, na Dan Ceballos wamepigwa faini na Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) baada ya kukutwa na makosa ya utovu wa nidhamu waliyofanya kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Atletico Madrid.

Kwa mujibu wa jarida la Football London la Aprili 4, 2025 Mbappe na Rudiger wamepigwa faini na kupewa adhabu ya kufungiwa mechi moja, lakini adhabu hiyo imesitishwa kwa mwaka mmoja yaani haitaanza kutekelezwa mara moja na itatekelezwa tu iwapo watarudia kosa ndani ya kipindi hicho cha mwaka mmoja.

Ceballos pia amepigwa faini kwa kosa hilo hilo, lakini UEFA haijafungua mashitaka yoyote dhidi ya Vinicius Jr, hivyo hajachukuliwa hatua yoyote.

Rudiger amepigwa faini ya dola 43, 838 (Sh117 milioni) wakati Mbappe atalipa faini kiasi cha dola 32, 878 (Sh88 milioni) huku Dan Ceballos akipigwa faini ya dola 21,919 (Sh58 milioni).

Wachezaji hao wanadaiwa kufanya matukio hayo baada ya Real Madrid kuibuka na ushindi wa penalti dhidi ya mahasimu wao Atletico Madrid katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora uliochezwa kwenye Uwanja wa Metropolitano.

Baada ya ushindi huo, baadhi ya wachezaji wa Madrid walionekana kufanya ishara ambazo zilitafsiriwa kama zisizofaa kwa mashabiki wa Atletico.

Rudiger anadaiwa kufanya ishara ya kukata koo, Ceballos alinaswa akifanya ishara chafu wakati akielekea vyumbani huku Mbappe naye akionekana akifanya ishara ya aibu alipotoka uwanjani. Hata hivyo, Vinicius Jr hajatajwa moja kwa moja kwenye tuhuma hizo.

Real Madrid imesema itawasilisha rufaa kupinga adhabu hizo lakini kwa sasa wachezaji wote wanne watakuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kwenda London kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Arsenal utakaochezwa Aprili 8, kwenye dimba la Emirates.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *