Mbappe aipeleka Madrid 16 bora kibabe

Madrid, Hispania. Mshambuliaji wa Madrid, Kylian Mbappe ameibuka shujaa baada ya kuifungia timu yake mabao matatu ‘hat trick’ katika mchezo wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa jana dhidi ya Man City kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.

Mbappe alifunga bao la kwanza katika dakika ya nne akimalizia pasi ya Raul Asencio huku bao lingine akifunga dakika ya 33 kabla ya kufunga lingine katika dakika ya 61 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Valverde.

Baada ya kufunga mabao matatu ‘hat trick’ Mbappe amehusika katika mabao 500 ya mashindano yote aliyocheza akiwa na timu ya taifa pamoja na klabu ambapo mpaka sasa ameshafunga mabao 358 na kutoa pasi za mwisho 142.

Madrid imefuzu katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa mabao 6-3 kwani katika mechi ya kwanza iliyochezwa England iliifunga Man City mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Etihad.

Baada ya kufuzu katika hatua ya 16 bora sasa Madrid inaweza kukutana na timu kati ya Bayern Leverkusen au Atletico Madrid katika droo itakayopangwa kesho huko Nyon, Switzerland.

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola kwa mara ya kwanza timu yake inaweka historia ya kuondolewa katika hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya mfumo mpya kuanza kutumika.

Katika michezo mingine iliyochezwa jana ilishuhudiwa PSG ikifuzu kibabe baada ya kuifunga Brest mabao 7-0 huku ikifuzu kwa jumla ya mabao 10-0 ambapo mechi ya kwanza ilipata ushindi wa mabao 3-0 ilipokuwa ugenini.

Juventus imeondolewa baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa PSV ambayo imefuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 kwani katika mechi ya kwanza iliochezwa Italia, Juventus ilishinda mabao 2-1.

Juventus sasa inaungana na AC Milan pamoja na Atalanta ambazo zinatoka Ligi moja ya Seria A nchini Italia huku Inter Milan ikiwa ndiyo timu pekee ambayo imefuzu katika hatua ya 16 bora.

Timu nyingine ni Borussia Dortimund ambayo imeungana na Bayern München pamoja na Bayern Leverkusern baada ya kupata sare ya 0-0 dhidi ya Sporting CP kwenye uwanja wa nyumbani huku ikifuzu kwa ushindi wa mabao 3-0 ilioupata ilipokuwa ugenini nchini Ureno.

Timu zilizofuzu katika hatua ya 16 bora

Zilizomaliza katika nafasi nane za juu 
Arsenal, Aston Villa, Atletico, Barcelona, Inter, Leverkusen, Lille, Liverpool

Zilizofuzu katika hatua ya mtoano
Borussia Dortmund, Bayern München, Benfica, Club Brugge, Feyenoord, Paris, PSV na Real Madrid