Mbalizi kuwa jimbo jipya la uchaguzi, wadau wapongeza

Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imependekeza kuanza mchakato wa kuchunguza, kugawa au kubadili jina la jimbo la Mbeya vijijini katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajia kufanyika Oktoba 2025.

Akizungumza katika kikao cha madiwani kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Erica Yegella, Ofisa Utumishi wa Wilaya hiyo, Daudi Mbembela amesema wamepokea barua kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kubadili jina la jimbo hilo.

Amesema kutokana na barua hiyo, wanapendekeza wilaya hiyo kugawanya jimbo hilo ambalo linaundwa na tarafa tatu za Utengule, Isangati na Tembela na kwamba wilaya hiyo ina vigezo vya kuwa na majimbo mawili.

“Hivyo, tunawasilisha mapendekeza ya jimbo jipya litakaloitwa Mbalizi litakalochukua mipaka ya tarafa za Usongwe na Isangati lenye kilomita za mraba 1,216, idadi ya watu 276,120, kata 18, vijiji 86, vitongoji 85.

“Lakini naomba kuwasilisha jimbo la Mbeya jipya litakaloanzishwa, litakalochukua tarafa ya Tembela likiwa na kilomita za mraba 1,216, idadi ya watu 95,137, vijiji 54, vitongoji 328 na kata 38, jimbo letu lina vigezo vya kuwa na majimbo mawili,” amesema Mbembela.

Diwani wa Kata ya Iwindi, Mfisile Nswila amesema wamekuwa na kilio cha muda mrefu, ambapo walihitaji kugawanywa kwa jimbo kwani hiyo ni sawa na hatua ya kimaendeleo katika kuwafikishia huduma wananchi.

“Hata mbunge aliyepo madarakani inampa ugumu kujulikana kwa kazi anayoifanya, jimbo letu ni kubwa mno, kinachofanyika kata moja, nyingine haijui, binafsi naunga mkono na kukubaliana na uamuzi huo,” amesema Nswila.

Hata hivyo, kuhusu taarifa za Mbeya Jiji kupoka baadhi ya maeneo ya Mbeya vijijini, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mwalingo Kisemba amesema hakuna mamlaka inayoruhusiwa kujadili mamlaka nyingine kisheria.

“Mamlaka moja haiwezi kujadili mamlaka nyingine hadi iwe na kibali, vinginevyo ni kosa kisheria, linahitaji kukemewa kama lipo, naamini wanajua hawawezi kufanya hivyo,” amesema Kisemba.

Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Oran Njeza amesema imekuwa ni kilio chake cha muda mrefu bungeni kuomba kugawanywa kwa jimbo kutokana na ukubwa wake pamoja na kupandisha hadhi mji wa Mbalizi.

“Eneo hili ni kubwa mno, limepakana na majimbo yote ya Mbeya na Songwe isipokuwa Kyela na Tunduma, fikiria kuna kitongoji kina watu 100,000, lakini shughuli za kiuchumi zinaongezeka,” amesema Njeza.

Mmoja wa wananchi katika Mji wa Mbalizi, Angella Mwasote amesema mgawanyo wa jimbo hilo ni kama umechelewa kwa kuwa wilaya hiyo ni kubwa na ongezeko la watu ni kubwa na wanahitaji huduma za kijamii.

“Huenda Mbeya Vijijini ndio jimbo kubwa kuliko yote mkoani Mbeya, kugawanywa kwake kutaleta tija kwa wananchi kufikiwa na huduma, tunaipongeza S­erikali kwa kuona hili,” amesema Angella.