Mbabe wa Diarra azidi kutupia, Makambo karudi kambani

BAO la dakika za jioni lililopachikwa kwa kichwa na Harittie Makambo, limeipa pointi moja Tabora United nyumbani ilipoikaribisha KenGold kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora.

Katika mchezo huo ulioanza kwa timu hizo kuheshimiana na kucheza kwa nidhamu, bao la kwanza lilipatikana dakika ya 27 lililofungwa na Seleman Bwezi kwa mkwaju wa penalti baada ya Obrey Chirwa kufanyiwa faulo eneo la hatari, kabla ya Makambo kusawazisha dakika ya 87.

Hilo ni bao la tatu la Bwezi akifunga mechi tatu mfululizo tangu alipomtungua Djigui Diarra kwa bao la kideoni akipiga mpira kutokea katikati ya uwanja zilipokutana KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, Yanga ikishinda mabao 6-1.

Bao la pili amefunga dhidi Fountain Gate kwenye ushindi wa mabao 2-0 ilioupata KenGold nyumbani Sokoine kwa mkwaju wa penalti na leo akifunga dhidi ya Tabora katika sare ya bao 1-1.

Makambo amefunga bao lake la tano akikwamisha mpira kambani kwa kichwa na hapo hapo kupata jeraha baada ya kugongana na beki wa KenGold huku mpira ukitinga nyavuni.

Sare hiyo imeifanya Tabora ifikishe pointi 32 na kubaki nafasi ya tano, huku KenGold ikiendelea kuburuza mkia kwa pointi 10.