
Katika siku ya kwanza ya ziara yake nchini Cuba, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa nchi hii katika masuala ya sayansi na teknolojia na kuzungumzia nyanja za maendeleo ya ushirikiano wa kisayansi, kiteknolojia na mawasiliano.
Eduardo Martinez, Naibu Waziri Mkuu wa Cuba katika masuala ya sayansi na teknolojia, amekutana na Sayyid Sattar Hashemi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran, mjini Havana, ambapo ameashiria maendeleo makubwa ya Iran katika Nyanja mbalimbali za sayansi na teknolojia na kutoa wito wa kuendelezwa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili katika nyanja za mawasiliano ya simu, huduma za posta na akili mnemba.
Naibu Waziri Mkuu wa Cuba amezitaja nyanja mbalimbali za maendeleo na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kuwa zinafaa sana na kusisitiza kuwa safari ya Waziri wa Mawasiliano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko mjini Havana itasaidia sana katika maendeleo na uhusiano kati ya Iran na Cuba.
Akirejelea irada ya viongozi wa ngazi za juu wa Iran na Cuba kwa ajili ya kustawisha zaidi uhusiano na ushirikiano katika nyuga mbalimbali, Martinez amesema kuwa kufuatia safari hiyo nchi mbili zitaingia katika zama mpya za uhusiano na ushirikiano.
Naibu Waziri Mkuu wa Cuba katika Masuala ya Sayansi na Teknolojia amesifu msimamo madhubuti wa Iran katika kutoa jibu kali kwa uchokozi wa utawala wa Kizayuni na kueleza shukurani na mshikamano wa serikali na wananchi wa Cuba na Iran katika kukabiliana na ubeberu wa kimataifa na utawala wa Kizayuni.
Baada ya mazungumzo hayo, kimefanyika kikao cha pamoja cha wawakilishi wa makampuni binafsi na maafisa wakuu katika uwanja wa mawasiliano na teknolojia ya habari wa Cuba na Waziri wa Mawasiliano wa Iran na ujumbe aliofuatana nao.