Mazungumzo Urusi-Ukraine: Hakuna kusitisha mapigano, bali mabadilishano ya wafungwa

Mazungumzo kati ya wajumbe wa Urusi na Ukraine, chini ya upatanishi wa Uturuki mjini Istanbul, yamemalizika Jumatatu, Juni 2, baada ya zaidi ya saa moja, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imetangaza.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo hayo yamedumu chini ya saa moja. Mazungumzo mapya kati ya Urusi na Ukraine mjini Istanbul yamemalizika saa sita mchana siku ya Jumatatu. Hapo awali, Uturuki, katika jukumu lake kama mpatanishi kati ya nchi hizo mbili katika vita vya wazi tangu Februari 2022, imehakikisha, kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, kwamba mkutano huo umemalizika “bila matokeo mabaya.” “Pande zote mbili zitatoa taarifa,” ameongeza Öncü Keçeli.

Kauli ya Ukraine ilikuwa ya haraka. Muda mfupi baadaye, Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Ukraine Sergei Kyslytsia amesema kwamba “upande wa Urusi umeendelea kukataa pendekezo la usitishaji vita bila masharti” wakati wa duru hii mpya ya mazungumzo ya moja kwa moja huko Istanbul. Urusi, kwa upande wake, inadai kuwa imependekeza usitishaji mapigano kwa sehemu. “Tumetoa pendekezo la jumla. Usitishaji madhubuti wa mapigano kwa siku mbili au tatu katika baadhi ya maeneo ya ya vita,” ameelezea kiongozi wa ujumbe wake, Vladimir Medinsky.

Kulingana na waraka wa Urusi uliotumwa Kyiv siku ya Jumatatu na kuchapishwa na mashirika ya habari ya Urusi, Kremlin inadai, kabla ya kusitishwa kwa mapigano yoyote ya kina, kwamba Ukraine iondoe wanajeshi wake kutoka mikoa minne ambayo Moscow inadai kuwa imetwaa. Urusi inataka “kuondoka kabisa” kwa wanajeshi w Ukraine katika mikoa inayokaliwa kwa sehemu ya Donetsk, Luhansk, Zaporizhzhia na Kherson kabla ya “kutekelezwa kwa usitishaji mapigano wa siku 30.”

Wafungwa wote waliojeruhiwa kuachiliwa

Mazungumzo haya ya Istanbul hata hivyo yamewezesha pande hizo mbili kufikia makubaliano ya kubadilishana wafungwa waliojeruhiwa na miili ya wanajeshi waliouawa. “Tumekubali kubadilishana wafungwa wote wa vita waliojeruhiwa vibaya na wagonjwa mahututi. Kundi la pili linajumuisha askari vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 25, kwa idadi kamili kila upande. Pia tumekubali kurejesha miili 6,000 kwa 6,000 ya wanajeshi waliouawa kwa kila upande,” Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov amesema.

Kyiv pia imependekeza mkutano mpya na Moscow mwishoni mwa mwezi Juni. “Tunapendekeza kwa upande wa Urusi kufanya mkutano mwishoni mwa mwezi, kati ya Juni 20 na 30. Hii ni muhimu ili kuendeleza mchakato wa mazungumzo,” Rustem Umerov ameambia wanahabari. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, kwa upande wake, amejitolea kuandaa mkutano mwingine, wakati huu ukiwaleta pamoja Rais wa Urusi Vladimir Putin, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, na Rais wa Marekani Donald Trump.

Kwa upande wake, Volodymyr Zelensky amehakikisha katika mkutano na waandishi wa habari kando ya mkutano wa kilele huko Vilnius, Lithuania, kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin “lazima asipate chochote ambacho kinaweza kuhalalisha uchokozi wake.” “Zawadi yoyote ingemwonyesha tu kwamba vita hulipa,” amebainisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *