Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya DRC na waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda yaliyokuwa yaanze hapo jana mjini Doha, Qatar, yameahirishwa kwa muda bila hata hivyo ya kutangazwa kwa tarehe nyingine, vyanzo kutoka pande hizo mbili vimethibitisha.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
M23 na serikali ya Kinshasa zilikuwa zimepangiwa kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na ya kwanza tangu kundi hilo kuchukua udhibiti wa miji mikubwa miwili mashariki ya Congo ya Goma na Bukavu.
Licha ya kwamba haikuwa wazi ni kwa nini mazungumzo hayo yamehairishwa, vyanzo kutoka pande zote vinasema hadi kufikia Jumatatu ya wiki hii, havikuwa vimepokea mwaliko rasmi.
Aidha vyanzo vilivyokaribu na mchakato wa mazungumzo hayo, mwishoni mwa juma lililopita, vilithibitisha wawakilishi wa pande hizo mbili walikutana juma moja nyuma kwa siri, bila kusema walijadiliana kipi hasa.
Maelfu ya watu wameripotiwa kufariki katika machafuko ya hivi punde mashariki ya DRC wakati mamia ya wengine wakiwa wamepoteza makazi yao.
Wachambuzi wa masuala ya kiusalama wamekuwa wakionya kwamba huenda mzozo huo ukasambaa na kuwa wa kikanda ukihusisha mataifa jirani kama vile Burundi na Uganda.