
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri jana Jumapili ilitoa taarifa na kusema kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Badr Abdelatty amefanya mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi na kujadiliana naye kuhusu shambulio la Israel la siku ya Jumamosi dhidi ya baadhi ya maeneo ya Iran.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeongeza kuwa, kwa mara nyingine tena Waziri Abdelatty amelaani vikali shambulio hilo la Israel na kusema ni la kichochezi, lakikubaliki na linahatarisha usalama wa eneo hili zima.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri vile vile ametilia mkazo udharura wa kutoruhusu kufanikiwa njama za Israel za kuzusha vita vikubwa na ametaka kuchukuliwe hatua za makusudi za kuepusha vita vya namna hiyo ambavyo vitakuwa na madhara yasiyotabirika.
Afisa huyo mkuu wa masuala ya kidiplomasia wa Misri vilevile amesema kuwa, nchi yake kwa kushirikiana na Qatar zinaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha vita vinasimamishwa kwenye Ukanda wa Ghaza, misaada kamili wa kibinadamu inafikishwa kwenye ukanda huo bila ya masharti yoyote hasa madawa na suala la kubadilishana mateka baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni, linafanikishwa.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuchukua hatua madhubuti na za haraka za kuhakikisha utawala wa Kizayuni unakomesha jinai zake huko Ghaza na Lebanon na kusisitiza kuwa, ingawa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipendi vita, lakini wakati huo huo iko imara katika msimamo wake wa kutoa majibu makali kwa jinai na uhalifu wowote inaofanyiwa na adui.