Mawakili wa Lissu waibua madai mapya

Dar es Salaam. Mawakili wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu wameibua madai mapya wakidai Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari wanaingilia kesi dhidi ya mteja wao kabla mahakama haijatoa uamuzi Mei 6, 2025.

Lissu aliyekamatwa na Jeshi la Polisi Aprili 9, 2025, akiwa wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, na kisha kuhamishiwa Dar es Salaam, anashtakiwa kwa makosa ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.

Mawakili hao, wakiongozwa na Peter Kibatala, wamedai Bashungwa na Johari kuzungumzia shauri hilo kwa kubainisha hoja ambazo wao walizitoa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu zinamuweka hakimu kwenye wakati mgumu na zinaweza kuathiri mteja wao kupata haki.

Lissu alifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yanayomkabili Aprili 10, 2025. Kwa sasa, kesi hizo zinaendelea kwa njia ya mtandao, mshtakiwa akiwa mahabusu katika Gereza la Ukonga.

Aprili 24, kesi zilipoitwa mahakamani, Jeshi la Polisi liliwazuia wananchi, wakiwemo wafuasi wa Chadema, kuzisikiliza, kitendo kilichoibua malalamiko kutoka kwa mawakili wa Lissu.

Kupitia mawakili wake, Lissu anapinga kesi hizo kusikilizwa kwa njia ya mtandao. Mahakama imepanga Mei 6, 2025, kutoa uamuzi iwapo kesi ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa YouTube inayomkabili Lissu iendeshwe kwa njia ya mtandao au mshtakiwa apelekwe mahakamani.

Katika mkutano na waandishi wa habari leo Jumamosi, Mei 3, 2025, jijini Dar es Salaam, wakili Kibatala kwa niaba ya wenzake zaidi ya 30 amesema waziri na AG kuzungumzia jambo hilo nje ya mahakama ni kuvunja sheria.

“Kuingilia hoja tulizotoa ndani ya mahakama na uamuzi wake unapaswa kutolewa Mei 6, 2025 wamemweka hakimu na mahakama inayosikiliza shauri hili katika mazingira magumu. Hivi itaamua nini? Vinginevyo tutaona kama yale aliyosema Waziri Bashungwa na Hamza.

“Wamemfanya hakimu awe na uoga akitoa uamuzi mwingine atahisi anaweza kwenda tofauti na mabosi wake. Tunatoa wito kwa viongozi wachunge ndimi zao. Madaraka ni mazuri, lakini sheria ni nzuri zaidi. Na wanawashauri wengi tu wa kisheria, inakuwaje hawawatumii?” amehoji Kibatala.

Hata hivyo, amesema kauli za viongozi hao zimewapa mbinu nyingine mpya ya kuipambania kesi hiyo.

Kauli za Waziri, AG

Waziri Bashungwa na Johari walipotafutwa leo, Mei 3, 2025 na Mwananchi kuzungumzia madai ya mawakili hao hawakupatikana.

Aprili 30, 2025, jijini Dodoma, Bashungwa alisema Serikali itaendelea kutumia mfumo wa Mahakama Mtandao kuwawezesha wafungwa na mahabusu kusikiliza mashauri wakiwa magerezani, hususan wakati wa viashiria vya matishio ya usalama, ili kulinda amani na mali za wananchi.

Wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kwenye Gereza la Isanga, Bashungwa alisema mfumo huo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha usalama na utoaji haki kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

“Jeshi la Polisi linapopata taarifa za kiintelijensia kuhusu uwezekano wa fujo, kama ilivyotokea hivi karibuni kutokana na matamko ya baadhi ya viongozi wa Chadema, linaweza kushirikiana na mahakama kuendesha kesi kwa njia ya Mahakama Mtandao. Hili linasaidia kudhibiti machafuko mitaani na bado haki inatolewa,” alisema.

Siku hiyohiyo, Johari akiwa bungeni aliwajibu waliokosoa utaratibu wa uendeshaji wa kesi dhidi ya Lissu akisisitiza hatua hiyo ilifanyika kwa mujibu wa sheria baada ya tathmini kufanyika.

Akizungumza wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2025/26, Johari alisema usikilizaji wa kesi kwa njia ya mtandao nje ya mahakama ni jambo lililopo kisheria.

Alisema yapo mazingira waliyoyabaini yaliyowafanya waje na uendeshaji wa kesi kwa njia ya kielektroniki nje ya mahakama.

“Mahakama ita-asses (tathmini) mazingira yaliyopo siku hiyo na kuona tusikilizeje kesi hiyo, hasa katika mazingira ambapo kwenye mitandao na social media (mitandao ya jamii) zinarushwa habari za ajabuajabu na za kutisha,” alisema.

Kususia chakula

Wakati huohuo, wakili Kibatala amesema kutokana na anayopitia mteja wao gerezani, amewaambia kuwa kuanzia Jumatatu amekusudia kususia kula chakula kushinikiza haki kutendeka.

“Natoa taarifa rasmi kwa umma mteja wetu Lissu ataanza kususia kula chakula, siyo kwa sababu nyingine, anataka haki itendeke. Pengine kuanzia siku ya Jumatatu tutatoa taarifa, lakini kwa sasa mjue atasusa kula chakula. Kitakachomtokea wala hatajali,” amesema na kuongeza:

“Lissu ni kiongozi na ni jabali kwenye suala la sheria. Ametufanya wengi kusomea sheria, na ni mtu ambaye haogopi kesi, hata sisi tusingekuwapo angeendesha kesi mwenyewe.

“Kwa hiyo atasusia kula chakula hadi hapo haki itakapotendeka. Haki ipi? Sitaki kufanya kosa alilofanya Mwanasheria wa Serikali, lakini mjue ni haki tunayoidai mahakamani.”

Amedai Lissu hajapewa nafasi ya kuongea na mawakili wake tangu ahamishwe kutoka Keko kwenda Gereza la Ukonga, hivyo wanapitia wakati mgumu kumuona mteja wao kuzungumza kuhusu shauri hilo.

“Tukifika hatupewi faragha kuonana, isipokuwa kuna simu anayotumia wakili na nyingine Lissu. Tunatazamana kwa kioo. Hata kusalimiana hatushikani mkono ila anaweka mkono wake kioo upande wa pili, na mimi upande mwingine kuonyesha upendo.

“Hata ndugu zake pia hawapati nafasi ya kumuona wala kuongea. Tunashangaa, kuna kanuni na taratibu zinazoelekeza na kutoa ruhusa kwa mtu kuongea na ndugu zake, lakini mteja wetu Lissu ananyimwa,” amedai.

Huku akitokwa machozi, Kibatala amesema hawatendewi haki katika kuwasiliana na mteja wao kwa mfumo wa kioo huku askari Magereza wakimlinda Lissu, wengine wakiwa kwa wakili.

Pia wanadai ananyimwa haki ya kuabudu, akitoa mfano wa Ijumaa Kuu, Pasaka na Jumatatu ya Pasaka.

Majibu ya Magereza

Akizungumzia madai hayo, Msemaji wa Jeshi la Magereza, Elizabeth Mbezi amekanusha akisema mtu yeyote akiwa gerezani ana haki ya kuongea na wakili wake.

Wakili Peter Kibatala akizunguma wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Mei 3, 2025. Kulia kwakwe ni mawakili wenzake. Picha na Sunday George

“Na kwa vyovyote huwezi kumuacha peke yake, lazima awe na ulinzi. Wanataka maisha gani? Hata suala la kuabudu gerezani wanaabudu. Kuna wachungaji wanaingia gerezani na kuna wanaowafundisha dini kulingana na madhehebu yao,” amesema.

Kuhusu madai ya kuzuiwa, Mbezi amesema; “Wao wanasema, lakini mwenyewe (Lissu) wamemuuliza anazuiwa? Hakuna haki anayonyimwa mtu akiwa gerezani. Haki zote anapewa. Hao wanaozungumza wamuulize mwenyewe kama anayimwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *