Maumivu wafanyabiashara Tanzania kuzuiwa kuingia Malawi, Afrika Kusini

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amechapisha video fupi katika mitandao yake ya kijamii ikionyesha shehena za ndizi zilizoharibika baada ya kuzuiwa kuingia katika nchi za Malawi na Afrika Kusini.

Bashe amechapisha video hiyo leo Jumamosi Aprili 19, 2025 ambapo amesema kuwa kama Serikali za Malawi na Afrika Kusini hazitobadilisha maamuzi na kutufungulia masoko basi na Tanzania itaendelea na hatua za kusitisha usafirishaji na biashara za bidhaa za kilimo na nchi hizi mbili.

“Hii ndio hali ambayo wafanyabiashara wetu wako nayo baada ya Serikali ya Malawi kuzuia mazao kuingia nchini kwao. Kuvumilia hili kama Serikali inayohangaika na sekta ya kilimo ni ngumu,” ameandika na kuongeza…

“Nafahamu kumekuwa na maoni mbalimbali lakini naomba niendelee kusisitiza kuwa hadi Jumatano hii inayokuja, kama Serikali za Malawi na Afrika Kusini hazitobadilisha maamuzi na kutufungulia masoko basi na sisi tutaendelea na hatua za kusitisha usafirshaji na biashara za bidhaa za kilimo na nchi hizi mbili.”

Ikumbukwe Alhamisi Aprili 17, 2025 Serikali ya Tanzania ilisema itazuia uingizaji wa mazao na bidhaa za kilimo kutoka nchi za Malawi na Afrika Kusini kuanzia Jumatano Aprili 23, 2025 endapo vikwazo kwa Tanzania miongoni mwa nchi hizo vitaendelea.

Taarifa hiyo ilitolewa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe Alhamisi Aprili 17, 2025 kupitia mitandao yake ya kijamii, huku akisema amefanya jitihada mbalimbali na nchi husika ili kuondoa vikwazo hivyo bila mafanikio.

“Serikali imepokea taarifa rasmi kuwa Serikali ya Malawi imezuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, yakiwemo unga, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi. Hatua hii imeathiri moja kwa moja shughuli za wafanyabiashara wetu wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi,” amebanisha Bashe.

Waziri Bashe aliwashauri wasafirishaji wote wa Kitanzania wanaosafirisha bidhaa za kilimo kuacha kupakia bidhaa hizo mpaka hapo Malawi na Afrika Kusini watakapobadilisha msimamo wao.

“Ninathibitisha kuwa kama waziri mwenye dhamana, nimewasiliana kwa njia mbalimbali na Waziri wa Kilimo wa Malawi bila mafanikio ya kupata majibu rasmi,” aliongeza.

Maoni ya wadau

Baadhi ya wadau wametoa maoni yao chini ya video iliyochapishwa katika kurasa wa Waziri Bashe wakionyesha shauku yao kama Watanzania kutokana na kitendo hicho.

“Sasa siyo wakati wa kulalamika tena, fungieni bidhaa zao ila na nchi yetu ijipange sekta ya viwanda iamke kuwe na usindikaji mkubwa wa matunda yapate soko yakiwa shambani ili tusiwe tunatesa wakulima wetu. Mfano zamani Arusha kulikuwa na kiwanda cha pombe za banana ndizi zilikuwa zina soko sana, ghafla zimekuja products (bidhaa) za ajabu zenye ladha ya banana na ndizi zimetelekezwa. Kabla ya ubaya kuwa ubwela iwe ubaya faida kwetu,” ameandika Sabina Aloyce.

“Inaumiza sana kupitia Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha ione namna kumfuta machozi huyu mhanga hata kwa kidogo, lakini huku tukiwapa haki yao ya msingi ya hiki walichofanya hawa majirani,” ameandika Ziaka Itala.

“Nashauri Serikali ifanye jitihada ya mikakati kutafuta masoko katika nchi zingine, Afrika ni kubwa sana na Malawi ni kama mkoa tu wa Tanzania, pengine hata Mwanza kubwa. Hawa jamaa wana ukorofi tu, mara mipaka yetu na wao Ziwa Nyasa wanajiongezea…I’m sure (nina uhakika) wao wanatuhitaji sisi kuliko sisi tunavyowahitaji,” amendika Eddie Malume.

“Mimi kama mkulima kwa kweli wametukosea sana. Asante waziri kwa hatua uliyoanza nayo. Wasije kusema hujawataarifu,” ameandika Kissa Kasongwa.

“Kufika Jumatano ni kutaka amani, huku wanatujeruhi, itafika hiyo siku tayari majeraha yashakuwa ni makubwa kwa wafanyabiashara,” ameandika Dotto Buteye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *