Mamia ya Maulamaa mashuhuri wa Kisunni wa nchini Iran wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kivitendo na Maulamaa wa Ulimwengu wa Kiislamu katika kukabiliana na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza.
Katika barua yao hiyo kuhusiana na kadhia ya Palestina, wanazuoni hao mashuhuri wa Kisunni wa nchini Iran wamesisitizia kuonyeshwa mjibizo wa wazi na wa hadharani kwa jinai za utawala wa Kizayuni.
Imeelezwa katika barua hiyo kwamba, hii leo dunia inashuhudia mauaji ya kimbari na watu kulazimishwa kuyahama makazi yao huko Ghaza, pamoja na matukio mengine ya kusikitisha na kuhuzunisha yanayojiri katika eneo hilo.
Barua hiyo ya maulamaa mashuhuri wa Kisunni nchini Iran imeeleza bayana kuwa, jinai za adui khabithi wa Kizayuni aliyejizatiti kwa silaha zinafanywa kwa uungaji mkono wa wazi wa Marekani na serikali kadhaa za Ulaya; na utawala huo dhalimu na makafiri wa Kimagharibi wanaouunga mkono hawajali upinzani wa wanazuoni wa Kiislamu, watetezi wa uhuru Waislamu na wasio Waislamu, na hata wa jumuiya za kimataifa zisizochukua hatua yoyote ya maana.

Sehemu nyingine ya barua hiyo imetahadharisha juu ya kupanuka kwa wigo wa vita katika maeneo mengine ya dunia na kueleza kuwa: kwa uungaji mkono unaotarajia kupata kwa serikali mpya ya Marekani na baada ya kuuhodhi kikamilifu Ukanda wa Ghaza, utawala wa Kizayuni utatakeleza mpango wa kuuhodhi kikamilifu Ukingo wa Magharibi pia na kuhitimisha mpango wa kuundwa nchi ya Palestina.
Wanazuoni mashuhuri wa Kisunni wa nchini Iran wamewataka wanazuoni wa Ulimwengu wa Kiislamu wachukue hatua za kivitendo kuonyesha upinzani na malalamiko yao dhidi ya hali ya kutisha na kusikitisha inayoendelea kushuhudiwa hivi sasa huko Ghaza.
Mashambulio ya kinyama ya askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni yaliyoanza tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Ukanda wa Ghaza, hadi sasa yameshawaua shahidi Wapalestina wasiopungua 43,799 na kuwajeruhi wengine 103,601…/