Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Shirikisho la Ubelgiji imeangaza mnamo Juni 17, 2025, kwamba imeomba mwanadiplomasia wa zamani wa Ubelgiji Etienne Davignon, kupelekwa katika Mahakama ya Jinai ya Brussels, kama sehemu ya uchunguzi wa mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani Patrice Lumumba (1961), muasisi wa uhuru wa Kongo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu mjini Brussels, Pierre Benazet
Etienne Davignon, 92, ndiye pekee ambaye bado yuko hai kati ya washukiwa kumi waliolengwa katika malalamiko ya “uhalifu wa kivita” yaliyowasilishwa mwaka 2011 na watoto wa Lumumba.
Miaka 64 baada ya kuuawa kwa Patrice Lumumba, Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo huru (DRC), Januari 17, 1961, mahakama ya Ubelgiji itaamua kama kesi itafunguliwa.
Familia ya Patrice Lumumba iliwasilisha malalamiko miaka 14 iliyopita, ambayo yalipelekea tume ya bunge ya uchunguzi na kisha kukiri rasmi wajibu wa Ubelgiji.
Hatua ya mwisho ya uchunguzi sasa inaendelea, huku kukifunguliwa siku ya Jumanne Juni 17 utaratibu rasmi: kikao cha jopola majaji. Nchini Ubelgiji, chombo hiki kinawakilisha hatua ya mwisho ya uchunguzi wa mahakama na kitabaini kama kuna “ushahidi wa kutosha”—yaani, ushahidi wa kutosha wa hatia—ili kuhalalisha kufunguliwa kwa kesi.
“Mateso, unyanyasaji wa kinyama, na kushiriki katika uhalifu wa kivita”
Katika kesi hiyo, ofisi ya mwendesha mashitaka imeomba kesi ya jinai “kwa mateso na unyanyasaji wa kibinadamu na kushiriki katika uhalifu wa kivita,” na hili ndilo litakaloamuliwa kuanzia leo Jumanne mbele ya jopo la majaji pekee kwa mshukiwa mmoja pekee anayesalia, Etienne Davignon, ambaye baadaye alikuja kuwa Kamishna wa Ulaya na alikuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Nje mwaka wa 1961.

Wakati malalamiko hayo yakiwasilishwa, katika maadhimisho ya miaka hamsini tangu kuuawa kwa Patrice Lumumba, Wabelgiji wengine tisa pia wanalengwa, wakiwemo sita ambao bado wako hai. Wanadiplomasia, maafisa wa polisi, wanajeshi… Wote walihusishwa kwa namna moja au nyingine na Ubelgiji kuunga mkono uasi ulioongozwa na Katanga, mkoa ambako Patrice Lumumba aliuawa.
Jaji mchunguzi alifanikiwa kupata muhtasari wa ushahidi katika kikao cha faragha mbele ya tume ya uchunguzi ya bunge. Ilipelekea kutambuliwa kwa wajibu wa kimaadili wa Ubelgiji na kisha kwa kwa radhi alizoomba Waziri Mkuu kwa niaba ya Ubelgiji miaka mitatu iliyopita.