‘Matumizi ya mifumo kuongeza usalama, uaminifu’

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema Zanzibar inaendelea kupiga hatua katika kuimarisha matumizi ya teknolojia ili kuongeza usalama na kukuza uchumi wa Taifa na jamii kwa jumla.

Abdulla amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa huduma ya kulipia mafuta kwa njia ya simu kupitia huduma ya lipia kwa simu ya Mixx by Yas uliofanyika Unguja Machi 2, 2025.

Amesema hatua iliyochukuliwa na Kampuni ya Zanzibar Petroleum Ltd ya kuanzisha huduma ya kulipia mafuta kwa njia ya simu kupitia mtandao huo, inadhihirisha wazi huduma zao zinawarahisishia kufanya malipo wateja wao.

“Zanzibar inazidi kupiga hatua katika masuala ya teknolojia, huu ni ushahidi kuna mabadiliko ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia,” amesema Hemed.

Amesema kuanzishwa kwa huduma ya kulipia mafuta kwa njia ya simu kutaimarisha usalama wa miamala ya kifedha, kupunguza utegemezi wa pesa taslimu na wananchi, kununua mafuta  kwa usalama, haraka na kwa ufanisi mkubwa kupitia simu zao za mikononi.

Hata hivyo, ameagiza kampuni hiyo kuhakikisha wanasimamia vipengele vyote vya usalama wa matumizi ya huduma ya lipia kwa simu katika vituo vya mafuta na kuhakikisha  wananchi watakaotumia huduma hiyo watakuwa salama na hawatopata athari yoyote.

Sambamba na hayo, ametoa wito kwa wauzaji wengine wa mafuta ndani ya Zanzibar kuiga mfano huo kwa kuwawezesha wateja wao kulipia huduma kwa njia ya kielektroniki ili kuisaidia Serikali kufikia kusudio lake la kuboresha ushirikishwaji wa kifedha.

Amewasisitiza wananchi kutumia huduma hiyo ipasavyo itakayosaidia kurahisisha malipo na kuweka uwazi wa miamala na usalama wa fedha zao.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mixx by Yas Kanda ya  Zanzibar, Azizi Said Ali amesema wako tayari kushirikiana na Serikali na taasisi nyingine katika kuhakikisha matumizi ya teknoloji yanaongezeka Zanzibar hasa katika ufanyaji wa malipo kwa njia ya kidijitali.

Azizi amesema pia,wapo tayari kushirikiana na Serikali kuboresha huduma za kijamii kama vile nishati ya umeme, maji na mafuta kwa kumuwezesha mteja kufanya malipo kwa njia ya kidijitali kwa kutumia simu ya mkono kupakuwa huduma anayoihitaji.

Meneja Mkazi Kanda ya Tanzania wa Kampuni ya Zanzibar Petroleum, Altaf Jiwan amesema wataendelea kutoa huduma nzuri, haraka na kwa ufanisi ili kukidhi malengo ya kubuniwa kwa huduma hiyo ya kulipia kwa simu ili kumrahisishia mteja kupata huduma kwa haraka, salama na wakati wowote.