Matumizi ya fedha za kigeni nchini sasa ni kaa la moto

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za mwaka 2025 ambazo zinazuia kutumika kwa fedha za kigeni katika malipo ya huduma yoyote ndani ya nchi.

Kanuni hizo pia zimeorodhesha maeneo manne pekee ambayo fedha za kigeni zinazoweza kutumia fedha za kigeni ambayo ni michango ya uanachama inayolipwa na Serikali kwa taasisi za kikanda zilizopo nchini, miamala inahusisha balozi na mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini.

Maeneo mengine ni mikopo ya fedha za kigeni inayotolewa na benki za biashara na taasisi za fedha zilizopo nchini na Malipo ya bidhaa katika maduka yasiyotoza ushuru.

Kanuni hizi zinatolewa wakati ambao Serikali ilipiga marufuku ya matumizi ya fedha za kigeni kuanzia Julai Mosi 2024 na tangu wakati huo imekuwa ikisisitiza marufuku hiyo kwa kusema matumizi ya fedha za kigeni kwa shughuli za ndani ni kuhujumu uchumi.

Juni mwaka jana Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akisoma hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025 alitangaza marufuku ya malipo ya huduma kwa kutumia fedha za kigeni kuanzia Julai Mosi 2024 huku akieleza mwongozo wa suala hilo utatolewa baadaye.

Dk Mwigulu alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokabiliwa na upungufu wa fedha za kigeni katika mwaka 2023/24 na baadhi ya Watanzania wanakuza tatizo hilo kwa kudai malipo au kufanya malipo ya bidhaa na huduma zinazotolewa ndani ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni yaani.

Alisema jambo hilo linasababisha kuongezeka kwa mahitaji yasiyo ya lazima ya fedha za kigeni na kuwanyima fursa watu wanaohitaji fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia bidhaa na huduma muhimu kutoka nje ya nchi.

“Kitendo cha kuuza bidhaa au huduma za ndani kwa kutumia fedha za kigeni ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, ambacho kinabainisha kwamba Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali pekee kwa malipo ya ndani ya nchi,” alisema Mwigulu na kuongeza.

Leo Machi 29, 2025, kupitia tangazo la Serikali Na. 198 kanuni hizi zimetangazwa huku zikielekeza  bei zote za bidhaa na huduma nchini kutangazwa kwa shilingi ya Tanzania.

Kifungu cha 3 cha kanuni hii inaelekeza kuwa mtu anapaswa kufanya muamala ndani ya nchi kwa kutumia shilingi ya Tanzania pekee.

“Kwa kuzingatia masharti ya kanuni ndogo ya 1, mtu anatenda kosa endapo atafanya yafuatayo, atalazimisha, atashiriki, atasaidia au kuwezesha upangaji bei ya bidhaa au huduma, yoyote nchini kwa kutumia fedha ya kigeni, atanukuu, atatangaza, atabainisha au kuchapisha bei ya bidhaa au huduma yoyote nchini kwa kutumia fedha ya kigeni,”

Pia kifungu hicho kinaeleza kuwa endapo mtu atalazimisha au kuwezesha malipo ya bidhaa au huduma yoyote nchini kufanyika kwa kutumia fedha ya kigeni au atakataa bidhaa huduma yoyote nchini kulipiwa kwa kutumia shilingi ya Tanzania sambamba na kupokea malipo ya bidhaa au huduma ndani ya nchi kwa kutumia fedha ya kigeni.

“Kwa madhumuni ya kanuni ndogo ya (1),“muamala” maana yake ni kunukuu, kutangaza, kubainisha, kuchapisha au kupanga bei au kulipa au kupokea malipo ya bidhaa au huduma ndani ya nchi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo katika upande wa miamala iliyoainishwa kuwa inaweza kulipwa kwa kutumia fedha za kigeni kanuni hizi zinampa waziri mamlaka ya kuongeza au kupunguza orodha ya miamala baada ya mashauriano na Gavana.

Katika upande wa mikataba kifungu 5.-(1) Mtu yeyote hataruhusiwa kuingia mkataba wa bidhaa au huduma kwa malipo ya fedha ya kigeni ndani ya nchi, isipokuwa kwa mkataba unaohusisha malipo yaliyoruhusiwa kwa mujibu wa masharti ya kanuni ya 4.

“(2) Bila kuathiri kanuni ndogo ya (1)- (a) malipo kwa ajili ya wafanyakazi, huduma au bidhaa zitakazonunuliwa nchini wakati wa utekelezaji wa mkataba yatafanyika kwakutumia shilingi ya Tanzania, isipokuwa kwa mikataba itakayoruhusiwa kwa mujibu wa kanuni ya 4,” amesema.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni ya 4(b) mkataba wowote wa utoaji wa bidhaa au huduma ndani ya nchi ulioingiwa kwa fedha ya kigeni kabla ya kuanza kutumika kwa Kanuni hizi utapaswa kufanyiwa marekebisho ndani ya muda wa mwaka mmoja tangu tarehe ya kutangazwa kwa Kanuni hizi.

“(3) Mkataba ambao hautafanyiwa marekebisho ndani ya muda ulioainishwa katika kanuni ndogo ya (2)(b) utakuwa batili isipokuwa pale ambapo Waziri atatoa idhini ya kuongeza muda usiozidi muda wa mkataba ulioingiwa.,” imeelezwa..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *