Matukio ya madereva bajaji kujinyonga yaacha maswali Mbeya

Mbeya. Mbeya imegubikwa na sintofahamu kufuatia vifo vya mfululizo vya waendesha bajaji watatu wanaodaiwa kujinga kwa sababu ya madeni na msongo wa mawazo.

Katika tukio la kwanza, Baraka Kapange ameripotiwa kujinyonga katika Mtaa wa Nkuyu, Kata ya Iganzo jijini Mbeya.

 Marehemu alidaiwa kushindwa kulipa deni la Sh60,000 za marejesho ya bajaji kwa bosi wake pamoja na kodi ya nyumba aliyokuwa akiishi na mke wake.

Inadaiwa kuwa akiba ya Sh48,000 aliyokuwa nayo aliicheza kamali (bonanza) na kupoteza.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nkuyu, Andrew Mwakarobo, amesema kabla ya kufariki dunia, Kapande aliacha ujumbe wa kuomba msamaha kwa mke na wazazi wake kwa uamuzi aliouchukua. Kapange ameacha mtoto wa miezi sita.

“Alitoa taarifa kwa mke wake na wazazi wake kuhusu deni hilo, lakini alikuwa anadaiwa kodi ya nyumba takribani Sh60,000 na alikuwa na akiba ya Sh48,000 ambazo aliicheza bonanza na kupoteza.

Usiku wa kuamkia Februari 9, mke wake aliporudi nyumbani akakuta amejinyonga kwa kamba iliyounganishwa na waya,” alisema Mwakarobo.

Tukio la pili lilitokea Machi 4, 2025 katika Mtaa wa Nyibuko, Kata ya Iyela, ambapo dereva wa bajaji, Isaya Edwin (26), alikutwa amejinyonga bila kuacha ujumbe wowote.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyibuko, Titusi Virumba amesema alipokea taarifa kutoka kwa mwenye nyumba wa marehemu na mara moja akawajulisha Polisi Kata ambao walifika na kuchukua mwili kwa uchunguzi zaidi.

“Sababu kubwa ni kukithiri kwa michezo ya bonanza, pool na kamali. Vijana wengi huingia tamaa na wanapokosa hufikia uamuzi wa kujitoa uhai. Naomba Serikali iingilie kati kunusuru vijana,” amesema Virumba.

Mke wa marehemu, Neema Johnson, amesema mume wake alipitia changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa bajaji mbili alizokuwa akitumia kwa mkataba. Alidaiwa kushindwa kufikia malengo ya wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri, jambo ambalo lilimletea msongo wa mawazo.

“Inaweza kuwa msongo wa mawazo kutokana na changamoto hizo. Kuna muda alinyang’anywa baada ya kumuazima mwenzake (deiwaka), kuendesha kwa muda, nyingine ni kutofikia malengo,” alisema Neema.

Tukio la tatu, lililotokea Kata ya Iduda, marehemu George Albert alikutwa amejinyonga ndani ya chumba alichokuwa akiishi, akiacha ujumbe kwa familia yake.

Diwani wa kata hiyo, Pishon Tarabhan, alisema kuwa marehemu aliamua kujitoa uhai baada ya kushindwa kumudu madeni aliyokuwa nayo mke wake kupitia vikundi vya Vicoba.

“Alikuwa mjasiriamali wa kawaida, kabla ya kufariki aliacha ujumbe kuwa mke wake anadaiwa Vicoba, hali ambayo hakuweza kuimudu, akaamua kujitoa uhai,” alisema Tarabhan.

Diwani wa Kata ya Iganzo, Daniel Mwanjoka amesema kujiua kwa vijana kunapoteza nguvu kazi ya Taifa na amehimiza watu wenye matatizo kufika katika ofisi za Serikali ili kusaidiwa.

“Ni kutokana na makundi wanayojiingiza au tamaa kwa namna fulani. Tunapoteza nguvu kazi ya Taifa. Nashauri kama mtu ana tatizo afike ofisi ya Serikali asaidiwe,” alisema Mwanjoka.

Naye Diwani wa Kata ya Iyela, Mussa Ismail, aliwaomba wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kuwa wawazi kwa viongozi wao wanapokumbwa na changamoto.

“Binafsi sijapata kwa undani taarifa hizo japo mwenyekiti wangu aliniambia kuwapo kwa tukio hilo. Niwaombe wananchi kuwa wawazi pale wanapokumbwa na changamoto na wasisite kufika kwa viongozi wao kuwasaidia,” alisema diwani huyo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa, alisema hajapata taarifa rasmi za vifo hivyo, lakini anafuatilia kwa wasaidizi wake ili kutoa ufafanuzi zaidi.

“Hayo matukio sijayapata, nilisikia moja la Uyole na la Iyela hivi karibuni, lakini kwa ujumla sijawa na taarifa rasmi. Nitafuatilia kisha nitatoa taarifa zaidi,” alisema Kamanda huyo.