Matibabu ya wastaafu NHIF yazua mgongano -3

Dar es Salaam. Ni mgongano wa masilahi, ndivyo inavyodhihiri katika huduma ya matibabu kati ya kundi la wazee wastaafu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Wakati wazee wakisisitiza wanastahili kuendelea kutibiwa bure kwa kuwa walichangia kwa miaka mingi wakati wa ajira zao, NHIF inapendekeza waanze kuchangia sehemu ya matibabu kutoka kwenye pensheni zao ili kupunguza mzigo kwa mfuko.

Ripoti ya NHIF inaonyesha kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024, wastaafu walitumia Sh85.7 bilioni, sawa na asilimia 13 ya malipo yote yaliyofanywa na mfuko ndani ya kipindi hicho, ikilinganishwa na mwaka wa 2022/2023 ambao walitumia asilimia 11 ya malipo yote.

Mbali na hilo, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2022/23 ilizungumzia kuhusu wastaafu kunufaika bila kuchangia, hivyo kuidhoofisha NHIF.

“Mfuko unagharimia matibabu ya wastaafu na wenza wao ambao hawachangii mfuko, jambo hili linadhoofisha mfuko kwa sababu matumizi ya wastani ya kundi hili ni Sh84.70 bilioni kwa mwaka,” ilieleza ripoti ya CAG, Charles Kichere, iliyotolewa Machi 28, 2024.

Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonyesha kuna wazee milioni 3.49 walio na umri zaidi ya miaka 60 nchini, lakini mpaka kufikia Desemba 2024 NHIF ilikuwa inahudumia wastaafu 121,797.

Kwa idadi hiyo ya wanaotibiwa na mfuko, nyaraka na ripoti za kila mwaka zinaonyesha hutumia fedha nyingi kutokana na wengi kuwa na magonjwa yasiyoambukiza (moyo, figo, ini, kisukari na shinikizo la damu) ambayo matibabu yake hugharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Hata hivyo, Sera ya Afya ya mwaka 2007 inatamka huduma za afya kwa wazee kuanzia umri wa miaka 60 ni bure, hivyo waliokuwa wakitibiwa na NHIF huendelea kupata matibabu bure baada ya kustaafu.

Mtazamo wa wazee

Kwa mtazamo wa wastaafu, wamekuwa wakichangia miaka mingi na hawakuugua. Kwa sasa hawana kipato lakini wanahitaji huduma za matibabu zaidi.

Mwalimu mstaafu, Aneth Danda (68), ni miongoni mwa wazee ambao hawachangii mfuko kwa sasa na anaendelea kutibiwa.

“Ninasumbuliwa na kisukari na shinikizo la juu la damu. Nimekuwa nikihudhuria kila mwezi hospitali kwa vipimo na kuwaona wataalamu wa afya. Nimefanya kazi miaka mingi, sikuwa naugua na sikutumia fedha zozote kwa matibabu, lakini sasa ndiyo nazitumia,” anasema.

Daudi Lyimo, injinia aliyestaafu miaka mitano iliyopita, anasema amekuwa akitibiwa mara kwa mara sasa tofauti na awali.

“Nikilinganisha miaka minane nyuma na sasa, nahudhuria zaidi hospitali. Kikubwa, shinikizo la juu la damu linanisumbua. Nilipostaafu waliniambia nirudishe kadi zote za wanufaika, nikabakiwa na yangu na mke wangu. Sikutibiwa nilipokuwa kijana wakati nachangia, lakini sasa ndiyo nahitaji zaidi huduma za kitabibu,” anasema.

Jane Mwambegele, mkazi wa jijini Mbeya, anasema ni ngumu wastaafu kuanza kukatwa fedha upya ilhali hata pensheni yao haitoshi.

“Binafsi napokea Sh300,000 kila mwezi. Ukiangalia gharama za maisha zimepanda, nitaweza vipi kuishi kama NHIF nao wataanza kunikata?” anahoji.

Erasto John (68), mkazi wa Ngara, mkoani Kagera, anasema baada ya kustaafu yeye na mke wake wameendelea kutibiwa.

“Kama nimechangia miaka 33 niliyofanya kazi, ingawaje bima ilikuja baadaye, inawezekana vipi ukaanza kunikata tena kwenye pensheni na sheria inasema sitakiwi kukatwa chochote? Huu ni mgongano,” anasema.

Kauli ya NHIF

Kwa mujibu wa NHIF, kundi la wastaafu limekuwa likihudumiwa kupitia fedha zinazokusanywa na mfuko katika mapato yatokanayo na uwekezaji, pasipo wao na wenza wao kuchangia baada ya kustaafu.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka, anasema gharama za matumizi kwa kundi hilo zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka kulinganisha na fedha zilizopo kwa ajili ya kulihudumia.

“Ili kuendelea kuhudumia kundi hili sambamba na kulinda uhai wa mfuko, imependekezwa kigezo cha uchangiaji kiongezwe kutoka miaka 10 hadi 15, pamoja na wastaafu kuchangia kiasi cha fedha kama michango kutoka kwenye pensheni zao, ili waendelee kupata huduma sawa na walivyokuwa wakipata wakiwa watumishi,” anasema.

Dk Isaka anasema kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24, wastaafu walitumia Sh85.7 bilioni, sawa na asilimia 13 ya malipo yote yaliyofanywa na mfuko ndani ya kipindi hicho, ikilinganishwa na mwaka wa 2022/23 ambapo walitumia asilimia 11 ya malipo yote.

Kuhusu magonjwa yanayoongoza kwa wazee kutumia fedha nyingi katika mfuko, anasema katika mahudhurio ya wagonjwa mwaka 2023/24, magonjwa 10 yaliyoongoza kwa wastaafu kuwa na mahudhurio mengi.

Magonjwa yanayoathiri zaidi wastaafu ni shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo, UTI, malaria, vidonda vya tumbo, magonjwa mengine ya mfumo wa mkojo, maumivu ya mgongo na magonjwa ya figo.

“Huduma zinazoongoza kwa kutumia fedha nyingi zaidi kuwatibu wastaafu katika mwaka wa fedha 2023/2024 ni pamoja na kusafisha damu, malipo ya ushauri wa daktari bingwa na dawa,” anasema Dk Isaka.

Dialisisi (kusafisha damu) kwa wiki mgonjwa hufanya mara tatu kwa gharama ya Sh150,000 kwa kila mzunguko, hivyo kufanya Sh450,000 kwa wiki kwa mgonjwa mmoja.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, Crispin Kahesa, anasema kwa kadri unavyokuwa na umri mkubwa, maradhi mengi yanajitokeza, yakiwamo saratani.

Dk Kahesa, ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Ocean Road, anasema takwimu za kidunia zinaonyesha kuanzia miaka 75, wazee wanaweza kupata saratani, huku wengi wakikabiliwa na maradhi mengine yakiwamo kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na matatizo ya mifupa kwa wanawake waliokoma hedhi kwa kukosa calcium.

“Mara nyingi wengi huugua kutokana na lishe duni na uwezo wa kupata matibabu huwa changamoto kwao. Wengine hupata maradhi ya akili, hivyo hutegemea zaidi watoto, ndugu na jamaa,” anasema.

Nini kifanyike?

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Isaka, anasema:“Mikakati iliyopo ni pamoja na kuendelea kuomba Serikali kuidhinisha muda wa uchangiaji kuongezwa kutoka miaka 10 hadi 15, pamoja na wastaafu kuchangia kiasi cha fedha kutoka katika pensheni zao ili kuendelea kutumia huduma.”

Mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati, amesema ustawi wa wazee waliolitumikia taifa ni muhimu, hivyo NHIF inatakiwa kutafuta njia nyingine za kuhakikisha fedha zinapatikana kuendeleza uhimilivu wa mfuko.

“Uhai wa mfuko si sawa na uhai wa watu. Wastaafu wameshaitumikia nchi hii na sasa wanakula pensheni zao ambazo ni ndogo mno kulingana na mishahara yenyewe, huwezi kukata kwenye pensheni zao.

“NHIF wajiangalie, wafanye marekebisho kwenye matumizi yao, si kila mtu anatafuta mahali rahisi kuchukua fedha. Wawaache wazee. Pensheni inawafanya waishi, hawafanyi kazi tena, halafu wanataka hicho-hicho kidogo si sawa,” anasema.

Dk Osati amependekeza NHIF ikae pamoja na na Wizara ya Afya na Serikali kujadili suluhisho la changamoto hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *