
Baada ya kufanyiwa rafu mbaya staa wa Crystal Palace Jean Philippe-Mateta, amesema kwa sasa anaendelea vizuri na anatarajiwa kurejea uwanjani hivi karibuni akiwa na nguvu zaidi.
Staa huyo alifanyiwa madhambi na kipa wa Millwall, Liam Roberts na kuwahishwa hospitali baada ya kupata jeraha kubwa kichwani wakati wa mchezo wa raundi ya tano ya Kombe la FA, jana.
Millwall walibaki pungufu kwenye mchezo huo kuanzia dakika ya 10 tu baada ya mwamuzi kumpa kipa huyo kadi nyekundu kutokana na madhambi hayo hatari aliyofanya.
Hata hivyo saa, chache tangu staa huyo apelekwe hospitali alitumia ukurasa wake wa Instagram kuwaambia mashabiki wake kuwa anaendelea vizuri na wasiwe na hofu.
“Nawashukuru wote kwa maombi yenu, naendelea vizuri na natarajiwa kurejea uwanjani hivi karibuni, nafikiri nitarudi nikiwa na nguvu kuliko ilivyokuwa mwanzoni. Napenda kuwapongeza wachezaji wenzangu kutokana na kiwango ambacho wameonyesha kwenye mchezo huu na kupata ushindi hili ni jambo zuri sana kwetu.”
Kwenye mchezo huo Palace ilifanikiwa kwenda hatua ya robo fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Bao la kwanza lilikuwa la kujifunga la Japhet Tanganga, huku mengine yakifungwa na Eddie Nketiah ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Mateta na Daniel Munoz.
Akizungumza baada ya mchezo huo Nketiah alisema: “Ni ajali mbaya kwa kuwa inahusisha kichwa, lakini tunaamini kuwa atatoka hospitali na kurejea akiwa na nguvu kubwa, tuendelee kumuombea.”
Timu nyingine zilizofuzu robo ni Manchester City, Preston, AFC Bournemouth na Aston Villa.