Matengenezo ya barabara ya Ifakara – Malinyi yaendelea

Malinyi. Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba amesema kazi ya uwekaji wa makaravati na kutengeneza tuta ili kurejesha mawasiliano ya barabara ya Ifakara – Malinyi inaendelea, licha ya changamoto ya kuongezeka kwa maji ya Mto Furua yaliyosababisha makaravati kusombwa.

Ameeleza kuwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zimechangia kujaa kwa mto huo, hali iliyosababisha uharibifu wa miundombinu, lakini jitihada za dharura zinaendelea ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya usafiri na usafirishaji. Barabara hiyo kuu iko chini ya usimamizi wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads).

Kwa mujibu wa Waryuba, eneo la barabara kuu ya Tanroads lililoharibika kwa sasa haliwezi kufanyiwa matengenezo ya moja kwa moja kutokana na kuongezeka mara kwa mara kwa maji ya Mto Furua.

“Hii barabara inayosimamiwa na Tarura (Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini) kazi inaendelea, japokuwa tunakumbana na changamoto mbalimbali za hali ya hewa.

“Mvua zinanyesha karibu kila siku, maji hujaa na wakati mwingine hupungua. Hata hivyo, Tarura na Tanroads wapo eneo la kazi na wanaendelea na jitihada za kurejesha miundombinu,” amesema Waryuba.

Ameongeza kuwa tayari baadhi ya magari yameanza kupita katika barabara hiyo, hatua ambayo imeanza kupunguza adha ya usafiri na usafirishaji kwa wakazi wa eneo hilo.

Kuhusu hali ya nyumba zilizozingirwa na maji, Waryuba, amesema baadhi ya wananchi wamelazimika kuzihama nyumba zao kwa muda ili kuepuka madhara baada ya makazi yao kuzingirwa na mafuriko.

“Kwa sasa wataalamu wangu bado wanaendelea kufanya tathmini ili kubaini idadi kamili ya wananchi waliolazimika kuhama. Hata hivyo, karibu wote wamekwenda kujihifadhi kwa ndugu zao.

“Hili ni jambo la kawaida katika maeneo yetu, kwani mara nyingi mafuriko yanapotokea wananchi huchukua tahadhari kwa kujihifadhi kwa jamaa na marafiki,” amesema Waryuba.

Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Antipas Mgungusi amesema mvua bado zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, lakini kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara inaendelea ili kuhakikisha wananchi wanaweza kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine bila matatizo makubwa.

“Nimetoka leo Malinyi na sasa nipo Dodoma. Hali niliyoiacha huko Malinyi siyo mbaya sana, kwa sababu wataalamu kutoka Tanroads na Tarura bado wapo eneo la kazi na wanaendelea kurekebisha kipande cha barabara kilichoathirika. Ingawa kumekuwa na changamoto ya kuongezeka kwa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, juhudi za kurejesha hali ya kawaida zinaendelea,” amesema Mgungusi.

Kuhusu nyumba zilizozingirwa na maji, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Antipas Mgungusi amesema alifanya ziara kukagua maeneo yaliyoathirika na kuzungumza na baadhi ya wananchi walioathiriwa.

Ameeleza kuwa tayari wengi wao wameshaondoka katika makazi yao kwa muda ili kupisha maji, na watarudi mara hali itakapokuwa salama.

“Nilifika katika maeneo hayo na kuzungumza na wananchi. Wengi wameondoka kwa muda ili kuepuka athari zaidi, lakini naamini hali ikitengemaa watarejea salama kwenye makazi yao,” amesema Mgungusi.

Mmoja wa wakazi wa Malinyi, Joseph Ligonja Ngunja ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za haraka katika kurekebisha barabara hiyo, hatua iliyowezesha magari kuanza kupita na kupunguza usumbufu kwa wananchi.

“Kweli hali ilikuwa mbaya, lakini kwa hatua za haraka iliyochukuliwa na Serikali imesaidia kurejesha mawasiliano, tayari magari machache yameanza kupita na matengenezo bado yanaendelea,” amesema Ligonja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *