
KOCHA wa Transit Camp, Stephen Matata amesema ana kazi kubwa ya kufanya ndani ya timu hiyo baada ya kushuhudia akipoteza michezo mitatu mfululizo tangu ateuliwe kukiongoza kikosi hicho Januari 13, mwaka huu akichukua nafasi ya Ally Ally.
Matata ameiongoza timu hiyo katika michezo mitatu kabla ya ule wa jana ugenini dhidi ya Polisi Tanzania na amepoteza yote tena bila ya kufunga bao lolote, akichapwa 1-0 na Biashara United, (3-0) v Stand United, kisha (4-0) v Geita Gold.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Matata alisema tangu amejiunga na timu hiyo changamoto anayopambana nayo ni katika maeneo yote muhimu kwa maana ya ulinzi na ushambuliaji hivyo, inamuhitaji muda kidogo japo ratiba siyo rafiki.
“Ni ngumu kupambana na hali hiyo katika kipindi hiki ambacho ligi inaendelea na tena ikiwa mzunguko wa pili, tutapambana kadri ya uwezo wetu michezo ijayo kuhakikisha tunasogea juu zaidi kwenye msimamo ili kukwepa janga la kushuka daraja.”
Kabla ya Matata kuchukua mikoba ya timu hiyo, ilikuwa ikikaimiwa na Emmanuel Mwijarubi na mbali na kuiongoza michezo mitatu, ila kijumla Transit imecheza 18, ikishinda miwili, sare minne na kupoteza 12, ikiwa nafasi ya 14 na pointi 10.
Kocha huyo ana kumbukumbu nzuri ndani ya kikosi hicho kwani alishawahi kukipandisha Ligi Kuu msimu wa 2004-2005, na baada ya hapo akafanya hivyo kwa Maafande wa Tanzania Prisons mwaka 2011, kisha msimu wa 2021-2022, akaipandisha Mbeya Kwanza.