
BAADA ya kuiongoza Transit Camp katika michezo saba tu ya Ligi ya Championship, aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Stephen Matata ameondoka katika timu hiyo, huku akiweka wazi sababu kubwa ni kutokana na matokeo mabaya aliyokuwa anayapata.
Akizungumza na Mwanaspoti, Matata alisema amefikia uamuzi huo kwa masilahi mapana ya timu hiyo kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo tangu amejiunga na kikosi hicho, huku akishukuru uongozi kwa kukubali na kuheshimu maombi yake.
“Niliamua kuwasilisha barua ya kujiuzulu mwenyewe kwa sababu ya matokeo mabovu ambayo nilikuwa nayo, kiukweli iliniumiza kama kocha lakini niliona ni muda wa kukaa pembeni na kuwaachia wengine nafasi ya kuendeleza pale nilipoishia,” alisema.
Katika mechi saba alizoiongoza timu hiyo, alishinda mmoja tu, sare mmoja na kupoteza mitano, akiiacha ikishika nafasi ya 15 na pointi zake 11, ingawa kiujumla imecheza michezo 24 na kati ya hiyo imeshinda miwili, sare mitano na kupoteza 17.
Kocha huyo anakumbukumbu nzuri ndani ya kikosi hicho kwani alishawahi kukipandisha Ligi Kuu msimu wa 2004-2005 na baada ya hapo akafanya hivyo kwa Maafande wa Tanzania Prisons mwaka 2011, kisha msimu wa 2021-2022, akaipandisha Mbeya Kwanza.