
Dar es Salaam. Msimu wa 2023/24, aliwaacha mbali Djigui Diarra wa Yanga na Mohamed Mustapha ‘Azam FC’ akitwaa tuzo ya kipa bora si mwingine ni Ley Matampi ambaye amesisitiza kuwa na msimu huu pia anaitaka.
Kipa huyo tayari ameruhusu nyavu zake kutikiswa kwenye michezo mitano kati ya mechi sita walizocheza lakini hilo amesema halimpi taabu kwani kwake ni bora kucheka mwisho na sio mwanzo.
Mwananchi limepata nafasi ya kuzungumza na Matampi akifunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutetea tuzo yake na kumtaja kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara kuwa ujio wake umeongeza vita mpya na hayupo tayari kuachia nafasi hiyo.
Camara ameongeza ushindani
Matampi amesema Camara amekuja Bongo kuongeza ushindani kwenye ligi, na kila mmoja lazima aheshimu uwezo wake kwa kuwa ni kipa bora ingawa hamfahamu sana.
“Ukiondoa ujio wa Camara, uwepo wa Diarra na Mustafa kuna makipa wengine wengi wanafanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara, ninachotakiwa kukifanya ni kuongeza juhudi ili kuendeleza ubora wangu na kujiweka kwenye ushindani.
“Natambua ubora wa kila mmoja na ujio wa Camara ambaye amejiunga na Simba unaendelea kuongeza chachu ya ushindani hasa kwenye eneo la makipa, namfahamu Diarra, Mustapha kwa sababu tulikuwa wote msimu ulioisha, ujio wa Camara unaongeza ushindani nitapambana zaidi ili nijiweke sehemu nzuri zaidi naamini yeye kaongeza vita tu kwenye ligi.”
Kutua Simba
Dirisha kubwa la usajili mengi yalizungumzwa kuhusiana na Matampi kutua Simba lakini haikuwa hivyo kipa huyo amefunguka sababu kuwa ni uongozi.
“Ni kweli kulikuwa na mazungumzo kati yangu na Simba kwa ajili ya kuitumikia msimu huu lakini mambo yalienda tofauti kutokana na viongozi wa Coastal Union kufanya mazungumzo na mimi ili kutoa uzoefu kwa vijana waliopo.
“Viongozi walikaa chini na mimi wakiniomba niendelee kusalia ndani ya Coastal Union ili niweze kuwafundisha vijana waliopo kutokana na uzoefu nilionao.”
Matampi anasema bado kuna muda kama ikitokea nafasi nyingine atafanya hivyo ila kwa sasa ni mchezaji wa Coastal Union haoni sababu ya kuzungumza masuala yaliyopita.
Wala hajali
Wakati wadau wengi wakiikatia tamaa Coastal Union kutokana na matokeo mabaya ya mechi nne za mwanzo wakipoteza zote Matampi amesema ni mapema sana.
“Sishtushwi japo sio mipango yetu lakini ukweli ni kwamba hata msimu uliopita nakumbuka mechi tano tulikuwa na pointi mbili hivyo kilichopo ni kuendeleza mapambano tu ili kuweza kufikia malengo,” anasema na kuongeza;
“Matokeo yaliyopo sasa yanatuumiza na hatufurahishwi na kinachotokea lakini tunaamini kila kitu kinawezekana tukiwekeza nguvu kwa kuongeza juhudi za mapambano uwanjani.”
Matampi ni mmoja
Licha ya kuachwa mbali na baadhi ya makipa ambao wanaongoza kwa kuzisaidia timu zao kutoruhusu mabao kwenye mechi walizocheza wakiongozwa na Mussa Mbisa (Tanzania Prisons) ambaye ameiongoza timu yake kwenye mechi nne bila kufungwa, Camara mechi tatu, kipa huyo amesema.
“Ni kweli kuna makipa tayari wameziongoza timu zao bila ya kuruhusu mabao hilo kwangu wala halinipi shida kwani naamini kwenye mwisho kuliko mwanzo, ninauwezo wa kutetea tuzo yangu kwani kuna mechi nyingi mbele.
“Nawapongeza makipa ambao tayari wameweka rekodi ya kutofungwa hadi sasa nawaambia kuwa mimi ni Matampi na nitabaki kuitwa hivyo, sishindani na mtu nashindana na mimi mwenyewe kwa kuweka malengo ambayo ni kujiweka kwenye nafasi ile ile ya msimu uliopita.”
Kimataifa safi
Matampi msimu huu ni wa pili kwake akiitumikia Coastal Union baada ya msimu ulioisha kuisaidia kumaliza nafasi ya nne na kushiriki michuano ya kimataifa amefunguka kuwa msimu ujao pia wanaitaka nafasi hiyo na hakuna kinachoshindikana.
“Ni mapema sana kuiondoa timu yetu kwenye nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa mimi bado naamini tuna nafasi hiyo na tunaweza endapo uongozi utawekeza nguvu.
“Uongozi ukiwekeza juhudi na jitihada zao zote kwa kuijenga timu vyema kisaikolojia na kutengeneza mazingira mazuri kuanzia juu hadi kwetu wachezaji hakuna kinachoshindikana na bado tuna michezo mingi ambayo inaweza kuturudisha kwenye ushindani.”
Kwanini hakucheza mechi za Caf
Awali ilikuwa inaelezwa kipa huyo alisaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Coastal Union na hatakuwa sehemu ya kikosi hicho msimu huu lakini mambo yameenda tofauti anaendelea kuitumikia timu hiyo, mwenyewe amefunguka sababu.
“Ni kweli kulikuwa na mgogoro wa kimkataba kutokana na kupishana na viongozi kwenye makubaliano lakini sasa nipo ndani ya timu baada ya kukaa nao na kumalizana kama ambavyo mimi nilikuwa nataka, sioni sababu ya kuzungumza mambo yaliyopita.
“Sababu ya mimi kuchelewa kujiunga na timu na kukosa baadhi ya michezo ya kimataifa ni kutokana na kutomalizana na viongozi na nimerejea baada ya makubaliano kwenda sawa, sasa acha kazi iendelee,” alimalizia