Mataifa yatoa wito wa kuwepo mkataba wa plastiki wenye nguvu

Mazungumzo hayo yalisambaratika mwishoni mwa 2024 huku mataifa yakishindwa kukubaliana jinsi ya kuzuia mamilioni ya tani za taka za plastiki kuingizwa katika mazingira kila mwaka.

Kabla ya duru inayofuata ya mazungumzo mwezi Agosti, mawaziri kutoka nchi 95 walitoa mwito wa kiishara wa kuwepo kwa mkataba wa kisheria ambao unazuia uzalishaji wa plastiki na kuondoa kemikali hatari.

Akizungumza katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari, waziri wa mazingira wa Ufaransa Agnes Pannier-Runacher ameyataka mataifa kutia saini tamko la Nice kuhusu uchafuzi unaotokana na plastiki. “Kwa nini tamko hili ni muhimu? Kwa sababu baadhi ya nchi zinajaribu kutufanya tuamini kwamba kwa kuchukua hatua kuhusu ukusanyaji, uchambuaji, na kuchakata tena, tutamaliza uchafuzi wa plastiki. Huu ni uongo. Hatuwezi, hatupaswi kuunga mkono uongo huu. Tunajua kwamba tusipofanya chochote, ifikapo mwaka wa 2060, uzalishaji wa plastiki utaongezeka mara tatu, na taka hizi za plastiki zitaongezeka mara tatu, na kutuzamisha ikiwa hatutachukua hatua.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari mjini Nice, Ufaransa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyahimiza mataifa “kukabiliana na janga la uchafuzi wa plastiki”. Picha: Bruno Bebert/abaca/picture alliance

Mataifa yanayoitwa yenye “nia kubwa” kwa muda mrefu yamesisitiza makubaliano hayo kujumuisha vizuizi katika utengenezaji wa aina mpya ya plastiki, ambayo kwa kiasi kikubwa imetengenezwa kutokana na kemikali zinazotokana na nishati ya visukuku.

Nalo kundi pinzani la nchi zinazojiita “zenye nia inayofanana” — nyingi zikiwa za kampuni kubwa za mafuta na kemikali zinazotokana na uchakataji wa mafuta — zimekataa wito wa kuwekwa ukomo wa uzalishaji, na badala yake kushinikiza kupatikana kwa mkataba ambao unatanguliza usimamizi wa taka.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyahimiza mataifa “kukabiliana na janga la uchafuzi wa plastiki”. “Nchi zote lazima zikamilishe haraka mazungumzo ya mkataba kabambe, wa kisheria wa kimataifa ili kukomesha uchafuzi unaotokana na plastiki. Na tunatumai kuwa hili litafanyika mwaka huu.”

Mnamo mwaka wa 2019, ulimwengu ulizalisha karibu tani milioni 460 za plastiki, takwimu ambayo imeongezeka mara mbili tangu mwaka wa 2000, kulingana na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo. Uzalishaji wa plastiki unatarajiwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka wa 2060.

AFP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *