Mataifa mbalimbali yaendelea kulaani hujuma ya Israel dhidi ya Iran

Mataifa mbalimbali yamendelea kutoa taarifa yakilaani hujuma za kijeshi za utawala wa Kizayuni Wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri sambamba na kulaani chokochoko hiyo yay Israel imesema kuwa, inakemea vikali hatua yoyote ile yenye kuhatarisha usalama na uthabiti wa eneo.

Umoja wa Falme za Kiarabu umelaani vikali shambulio hilo la kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuendelea mvutano huo na matokeo yake katika usalama na uthabiti wa eneo hili.

Kwa upande wake Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan iliyachukulia mashambulizi ya kivamizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran kuwa ni ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala na kuvunja sheria za kimataifa na kusababisha kushadidi mivutano katika eneo.

Kabla ya hapo pia, Wizara za Mashauri ya Kigeni za Saudi Arabia na Oman zililaani kitendo cha kichokozi cha utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kukiona kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Idara ya Mahusiano ya Umma ya Ulinzi wa Anga wa Iran ilitoa taarifa ikisema kuwa jana Jumamosi alfajiri utawala wa Kizayuni wa Israel ulishambulia vituo vya kijeshi vya mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam ikiwa ni katika kuzidisha hali ya mvutano katika eneo, ambapo mfumo wa ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeweza kukabiliana kwa mafanikio na kitendo hicho cha kichokozi cha utawala wa Kizayuni.