Dar es Salaam. Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa Usimamizi wa Rasilimali za Usafiri utakaofanyika jijini Arusha kuanzia Aprili 9 hadi 11, 2025.
Mkutano huo umeandaliwa na Chama cha Barabara Duniani (PIARC) kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, kupitia Chama cha Barabara Tanzania (Tara).
Utawahusisha washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi 35 duniani, wakiwemo wataalamu kutoka Marekani, Uswisi, Ufaransa, Namibia, India, Estonia, Ghana, Australia, Afrika Kusini, Ureno, Japani, New Zealand, Argentina, Chile, Tunisia, Uingereza, Msumbiji na mataifa mengine.
Mkutano huu ni miongoni mwa mikutano mingi ya kimataifa iliyofanyika nchini tangu 2021, ikiakisi juhudi za Serikali katika kuimarisha diplomasia na utalii wa mikutano.
Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza umuhimu wa Tanzania kushirikiana na mataifa mengine kukuza ushirikiano wa kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tara, Joseph Haule alisema Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega atakuwa mgeni rasmi wa mkutano huo.
“Pia mkutano huu unakwenda kuwakutanisha viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau na watumiaji wa vyombo vya usafiri,” amesema Haule.
Haule amebainisha kuwa matarajio ya mkutano huo ni kubadilishana maarifa kutoka mataifa mbalimbali ikiwamo kusambaza mbinu bora na kukuza uwezo katika usimamizi wa rasilimali za usafirishaji katika kila nchi.
Aidha, Haule alisema mkutano huo pia utakuwa fursa kwa Tanzania kujifunza kutoka kwa mataifa yaliyoendelea katika sekta ya barabara, hususan Namibia, ambayo ina miundombinu bora zaidi ya usafirishaji barani Afrika.
Akibainisha changamoto kubwa zinazoikumba miundombinu na rasilimali za usafirishaji katika nchi nyingi za Afrika, amesema ukosefu wa fedha za ujenzi na mabadiliko ya tabianchi ndio chanzo cha athari mbalimbali ikiwamo kuyumba kwa uchumi wa nchi husika.
Alipoulizwa kuhusu ucheleweshaji wa miradi ya ujenzi na uwezekano wa kuweka mfumo wa kuwathamini zaidi makandarasi wazawa kwa kuwapa fursa katika miradi hiyo, alieleza kuwa hayo ni miongoni mwa masuala nyeti yatakayojadiliwa katika mkutano huo ili kutafuta ufumbuzi.
Aidha, alibainisha kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria za matumizi ya barabara, akitaja changamoto za kibinadamu zinazohusiana na matumizi mabaya ya miundombinu, hali inayosababisha uharibifu wa rasilimali na kuhatarisha maisha, hususan kwa waendesha pikipiki.

Alitoa mifano ya baadhi ya maeneo kama madaraja ya Kijazi na Mfugale pamoja na kivuko cha Buguruni, ambako baadhi ya wakazi hujaribu kuvuka sehemu zisizoruhusiwa, jambo linalosababisha ajali na vifo.
Licha ya Serikali ya Tanzania kuweka sharti kwamba barabara zote mpya zinazojengwa kwa kiwango cha lami lazima zijumuishe njia za waenda kwa miguu katika majiji, miji na maeneo mengine, changamoto bado zipo katika maeneo mengi.
Akizungumzia suala hilo bungeni Februari 5, 2025, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya alisema kuna sheria mahsusi zinazopaswa kufuatwa na watumiaji wote wa barabara.
Kuhusu waendesha pikipiki wanaokiuka sheria, Kasekenya alisisitiza suala hilo linashughulikiwa na vyombo husika.
“Sheria zipo na zinatumika kuhakikisha kila mtumiaji wa barabara anafuata taratibu zilizowekwa. Waendesha pikipiki wanaovunja sheria wanachukuliwa hatua na mamlaka husika,” alisema naibu waziri huyo.